Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Jukwaa la Taifa la Wanawake Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Lazinduliwa
Nov 29, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) limezindua Jukwaa la Taifa la Wanawake wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania 28 Novemba, 2021, ambapo litawawezesha wanawake kupaza sauti zao kwenye sehemu husika na kuweza kusikika kwa haraka na sauti zao kufanyiwa kazi.

Jukwaa hilo limezinduliwa jijini Mbeya na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge, Bw. Kaspar Mmuya ikiwa ni kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani Desemba Mosi yakiwa na kauli mbiu ya “Kuzingatia Usawa, Kutokomeza Ukimwi, Kutokomeza magonjwa ya mlipuko”.

Akihutubia wakati wa uzinduzi huo alisema, baraza hilo limekuja wakati sahihi kwa kuzingatia malengo yake katika kuhakikisha kunakuwa na sauti moja katika masuala yanayowahusu na kuathiri ustawi wao.

“Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU limekuwa chachu ya maendeleo na mabadiliko ya kisera, miongozo, sheria na utekelezaji wa afua mbalimbali za UKIMWI nchini, hongereni kwa kazi mnayoifanya”.

Naibu alieleza Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada hizo ili kuhakikisha malengo yake yanatimia kwa viwango vinavyotarajiwa.

“Serikali ipo tayari na itaendelea kushirikiana na Baraza la Watu wanaoishi na VVU pamoja na Jukwaa la Taifa la Wanawake wanaoishi na VVU nchini ili kuleta ufanisi katika mwitikio wa UKIMWI.”alisema Mmuya.

Akieleza historia ya uanzishwaji wa jukwaa hilo Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa alibainisha malengo yake ikiwemo kuleta utetezi wa wanawake WAVIU ili kuweza kupata haki zao za msingi, ushirikishwaji katika tafiti mbalimbali zinazofanyika nchini hasa kuhusu njia za kupunguza maambukizi na kupata taarifa zinazohusu kundi hili, kuwajengea wanawake uwezo, kujikubali na kujitambua katika kuwapa ujasiri.

Malengo mengine ni pamoja na kupata fursa za kushiriki kikamilifu katika shughuli za mwitikio wa UKIMWI katika ngazi mbalimbali, ushirikishwaji wa moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi pamoja na kupata nafasi za utetezi wa kundi hili katika kuhakikisha wanapatiwa haki zao za msingi ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya nchini.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa NACOPHA, Bi.Leticia Mourice alisema, uwepo wa jukwaa utasaidia kuchochea dhana ya ushirikishwaji wa wanawake WAVIU katika masuala yanayowahusu ili kujiletea maendeleo yao na kuwawezesha kutambua fursa na kushiriki kikamilifu katika masuala ya mbalimbali.

Sambamba na hilo, alisema Jukwaa hilo limeundwa kufuatia marekebisho ya Katiba ya Baraza yaliyofanyika mwaka 2013, ulionekana umuhimu wa kuwa na Jukwaa la Wanawake wanaoishi na maambukizi ya VVU kama ilivyoainishwa kwenye Sura ya Sita Ibara ndogo ya 2 na ya 6, ambayo inaelezea kuwa Baraza litakuwa na wajumbe wa Bodi kutoka Jukwaa la Wanawake WAVIU na Jukwaa la Vijana WAVIU.

“Kuundwa kwa Jukwaa hili kumetoa mwanga wa kuongezeka kwa wigo mpana wa kuwashirikisha wanawake WAVIU katika masuala yanayohusu maisha yao, kwa masalahi yao na jamii kwa ujumla. Jukwaa hili litatoa nafasi muhimu ya ushirikiano miongoni mwa wanawake WAVIU kupaza sauti zao katika mtazamo chanya wa umoja na upendo,”alieleza Leticia.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge masuala ya UKIMWI Mhe. Fatma Taufiq alipongea jitihada hizo na kuahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha mipango na mikakati yao inafikiwa na kutambulika kama ilivyokusudiwa.

Alitumia fursa hiyo kuwaasa wanawake nchini kujiamini, kujitambua na kujua nafasi zao ili kutoishi kwa matumaini bali kwa malengo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi