[caption id="attachment_16625" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya hiyo leo jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ardhi Kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni Chachu ya Maendeleo, Halmashauri Zitenge Ardhi kwa Ajili ya Uwekezaji wa Viwanda Vidogo na Vikubwa”. (Picha na: Frank Shija)[/caption]
Na: Paschal Dotto
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watendaji wa Serikali za Mitaa kusimamia wananchi wao kulipa kodi ili kuimarisha huduma za jamii kwa watanzania kwani kodi itaongeza mapato na kuboresha huduma za jamii.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa, (ALAT) Rais Magufuli amesema kuwa ili nchi iweze kuendelea kiuchumi lazima wananchi wake walipe kodi kwani hicho ni miongoni mwa chanzo muhimu cha mapato ya Serikali kinachoiwezesha kuwapatia wananchi huduma nzuri na bora.
“Tulianza kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma, tulibana mianya ya ukwepaji kodi na kuongeza ukusanyaji mapato kutoka bilioni 800 kwa mwezi hadi trilioni 1.3 kwa mwezi” Rais Magufuli alieleza.
Alifafanua kuwa kutokana na ongezeko hilo Serikali sasa inaweza kulipa mishahara kwa wakati huku ikilipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo ilikuwa inaidai Serikali shilingi trilioni 1.3 ambapo hadi sasa imeshalipwa shilingi trilioni 1.2.
Rais Magufuli alieleza kuwa katika utendaji kazi wa ALAT mkutano huo ni muhimu kwa serikali anayoiongoza kwani Jumuiya hiyo ni mhimili muhimu wa kuwaunganisha wananchi na serikali yao hivyo mkutano huo kwa nchi yetu una umuhimu wa kipekee.
“Kwangu mimi mkutano huu ni muhimu sana kwa sababu ALAT ni chombo kinachounganisha mamlaka na wadau wanaohusika na masuala ya Serikali”, alisisitiza Rais Magufuli.
Akibainisha miradi iliyotekelezwa mpaka sasa kutokana na mapato ya wananchi, Rais Magufuli alisema kuwa huduma ya elimu imeboreka zaidi baada ya serikali kuanza utaratibu wa kutoa shilingi bilioni 18 kwa mwezi katika mwaka wa fedha 2015-2016.
Kufuatia hatua hiyo alisema idadi ya watoto waliojiandikisha kuingia darasa la kwanza ilifikia asilimia 95 huku kidato cha kwanza wanafunzi wakiongezeka kwa asilimia 30 ambapo alisisitiza kuwa uwezo huo umetokana na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato.
Rais Magufuli aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa katika kutekeleza mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuimarisha miundombinu, serikali imeshatia saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora Dodoma, ambapo kwa awamu ya kwanza imeanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro. Mradi huu mkubwa utagharimu kiasi cha fedha za kitanzania shilingi trilioni 7.062 ambazo kwa asilimia 100 ni fedha za serikali kutoka kwa wananchi walipa kodi.
Alitaja miradi mingine kuwa ni upanuzi wa bandari mbalimbali za mizigo zikiwemo bandari za Mtwara bilioni 130, Dar es Salaam bilioni 926.2, Tanga bilioni 16 pamoja na ukarabati wa meli za mizigo katika Ziwa Nyasa na Ziwa Viktoria ambapo pesa zote hizo ni za serikali kwa asilimia 100.
Akijibu risala ya ALAT, Rais Magufuli ameipongeza Jumuiya hiyo na kuwataka wapambane na wasiogope katika kutenda na kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.
Naye Mwenyekiti wa ALAT, Gulamhafeez Mukadam ameiomba Serikali kutenga na kupeleka kwa wakati ruzuku katika Halmashauri zao ili waongeze ufanisi katika kazi ya kuwatumikia wananchi na kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Kauli mbiu ya mkutano huo wa 33 ni “Ardhi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ni chachu ya maendeleo, Halmashauri zitenge ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa” ambapo Mukadam alisema kuwa kauli mbiu hiyo inakwenda sambamba na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda.
ALAT ilianzishwa 1984 kwa lengo la kuwakutanisha pamoja watendaji wa Serikali za Mitaa ili waweze kubadilishana uzoiefu masuala ya utendaji kazi.