Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kushika nafasi ya nne barani Afrika kwa ubora wa usalama wa usafiri wa anga kupitia ukaguzi uliofanywa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) kwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kwa mwaka 2023.
Akizungumza jijini Dodoma mara baada kupokea taarifa ya Uendeshaji wa Viwanja vya Ndege nchini, Mhe. Kakoso amesema pamoja na huduma bora zinazotolewa katika Kiwanja cha JNIA, TAA iongeze ubunifu zaidi ili kuvutia mashirika mengi zaidi kutumia kiwanja hicho ili kuchochea uchumi kupitia usafiri wa anga nchini.
“Nawapongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya viwanja vya ndege kwani matokeo tayari yameanza kujionyesha kupitia kaguzi zinazofanywa na ICAO, hatua hii ionyeshe umuhimu wa kuwekeza zaidi ili mashirika yaongezeke na tuendelee kuaminika zaidi”, amesema Mhe. Kakoso.
Mhe. Kakoso ameitaka TAA kuhakikishia inaharakisha zoezi la kutafutia hati viwanja vyote nchini ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na wananchi kuvamia na kujenga katika maeneo ya viwanja nchini.
Aidha, Mhe Kakoso ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kutenga fedha kwa maeneo ambayo hayana viwanja vya ndege ili kurahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia usafiri wa anga kwani Serikali imeendelea kununua ndege mpya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha viwanja vyote nchini vinatoa huduma bora na znazokidhi viwango vilivyowekwa kimataifa kulingana na vigezo vya ICAO.
Naibu Waziri Mwakibete ameongeza kuwa kwa sasa Serikali inaharakisha kukamilisha mradi wa ufungaji taa kwa kiwanja cha ndege cha Dodoma ili kukiwezesha kiwanja hicho kutumika saa 24 ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Hamisi Amiri ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha za maboresho katika miundombinu ya viwanja vya ndege nchini na kuahidi kuwa mapendekezo yote ya kamati yatafanyiwa kazi kwa maendeleo ya sekta ya usafiri.wa anga nchini.