Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JKCI Yatenga Bilioni 66.3 Kuimarisha Huduma za Kibingwa
Jul 18, 2023
JKCI Yatenga Bilioni 66.3 Kuimarisha Huduma za Kibingwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa mkutano wa kuelezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na kutoa mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dar es Salaam.
Na Paschal Dotto-MAELEZO

Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imetenga shilingi bilioni 66.3 zitakazotumika katika utekelezaji wa kazi mbalimbali za kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kugharamia utendaji kazi wa taasisi hiyo ambayo ni muhimu kwa wananchi.

Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge amesema kuwa JKCI ni inatoa huduma ndani na nje ya nchi hivyo kuimarika kwa taasisi hiyo kupitia bajeti  ni jambo la kuongeza huduma na kufanya wageni waje kutibiwa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa mkutano wa kuelezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na kutoa mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dar es Salaam.

“Fedha tulizopata kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 tutazitumia kulipa wafanyakazi, uendeshaji wa gharama za Taasisi, manunuzi ya vifaa tiba, kusomesha wataalam wetu lakini pia zitatumika kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la uchunguzi wa wagonjwa ili kuimarisha huduma za kibingwa nchini."

Dkt. Kisenge alisema kuwa Serikali imeimarisha mambo mengi kwenye sekta ya afya ikiwemo ununuzi wa mashine za kibingwa na hiyo ilisababisha wagonjwa 301 kutibiwa kutoka nje ya nchi kwa nchi za Somali, Malawi, Kenya, Rwanda, Uganda, Zambia, Visiwa vya Comoro, Ethiopia, Burundi na wengine kutoka nje ya Afrika kwa nchi za Armania, China, India, Marekani na Uingereza.

Aidha, Dkt. Kisenge alisema kuwa Taasisi ilitumia shilingi bilioni 1.2  kwa ajili ya kununua mashine mbalimbali zikiwemo za utasishaji wa vifaa vya Hospitali, Digital X-Ray na mashine tatu za kuangalia jinsi moyo unavyofanyakazi (Echocardiography).

Ili kuimarisha huduma kwa wananchi JKCI imeanzisha huduma zijulikanazo kama Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services na Taasisi ilifanya upimaji wa moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Pwani, Arusha, Geita, Iringa, Mtwara, Lindi, Unguja, Manyara na Pemba na kupima zaidi ya wananchi 6,309 kati ya hao 3,239 walikutwa na matatizo ya moyo na kupewa rufaa ya kutibiwa JKCI.

Dkt. Kisenge aliongeza kuwa ili kuepuka na hatari ya kupata magonjwa ya moyo wananchi wanashauriwa kufanya mazoezi, kuepuka kula vyakula vya mafuta na chumvi nyingi pamoja na kupima afya ya moyo kila mara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi