Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia wanatarajia kufanya upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na kubadilisha valvu (milango ya moyo) zaidi ya miwili kwa wagonjwa 20.
Wagonjwa ambao wanabadilishiwa valvu na kuwekewa za bandia ni wale ambao valvu zao hazifanyi kazi vizuri na hivyo kuufanya moyo kushindwa kufanya kazi yake vizuri.
Kambi hii ya siku saba ilianza tarehe 09/09/2018 na inatarajiwa kumalizika tarehe 15/09/2018 inaenda sambamba na utoaji wa elimu na kubadilishana ujuzi wa kazi kati ya wafanyakazi wa Taasisi hizi mbili. Aidha wageni nao wamepata muda wa kujifunza vitu vingi na kupata uzoefu mpya wa baadhi ya magonjwa ambayo katika nchi yao hakuna.
Tangu kuanza kwa kambi hii hadi jana tarehe 12/09/2018 tumefanya upasuaji na kubadilisha valvu kwa wagonjwa 11 ambao hali zao zinaendelea vizuri na wengine wameruhusiwa kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kurudi wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi.
Kwa upande wa matumizi ya damu wakati wa upasuaji mgonjwa mmoja anatumia kati ya chupa tano hadi saba lakini kama mgonjwa atapata tatizo anaweza kutumia chupa zaidi ya hizo. Tunawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kuchangia damu ili wagonjwa wenye matatizo ya moyo waweze kufanyiwa upasuaji kwa wakati.
Aidha tunaendelea kuwasistiza wananchi wajiunge na mifuko ya bima za afya wangali na afya njema wasisubiri kujiunga na mifuko hiyo wakati wagonjwa kwani gharama za matibabu hasa ya moyo ni kubwa na wakijiunga na mifuko hiyo itawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapougua na kuhitaji kupata matibabu.
Kwa namna ya kipekee tunaishukuru sana Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) kwa kutuma wataalam wake wa magonjwa ya moyo kuja hapa nchini kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa wetu. Hakika Mwenyezi Mungu atawalipa kwa huduma hii mliyoitoa.
Hii ni mara ya pili kwa IIRO kuja kufanya kambi ya matibabu ya moyo katika Taasisi yetu. Kwa mara ya kwanza walikuja mwishoni mwa mwaka jana na kufanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono. Katika kambi hii jumla ya wagonjwa 33 walipata matibabu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
13/09/2018