Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JKCI Yaanzisha Kliniki ya Maumivu ya Kifua
Nov 21, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha kliniki ya matibabu ya maumivu ya kifua kwa wagonjwa wenye maumivu ya vichomi kifuani na kifua kubana ili waweze kufanyiwa uchunguzi wa haraka kwani maumivu hayo huambatana na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo shambulio la moyo.

Akizungumzia leo kuhusu kliniki hiyo inayofanyika JKCI iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo wa Taasisi hiyo, Dkt. Tatizo Waane alisema kuwepo kwa huduma hiyo kutawafanya wagonjwa kupata huduma ya matibabu mapema.

Dkt. Waane ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema maumivu ya kifua yamekuwepo katika jamii lakini maumivu hayo mara nyingi yamekuwa hayatambuliki kutokana na jamii inavyofikiria kwani mtu anapoumwa kifua hudhani ana matatizo ya nimonia au matatizo mengineyo bila kuhisi kuwa maumivu hayo yanaweza kuwa ni dalili za magonjwa ya moyo.

“Ninawaomba wananchi wote kutokudharau pale wanapopata maumivu ya kifua bali wapende afya zao na kuwa na utaratibu wa kupima afya pale wanapojisikia kuwa na maumivu ya kifua”, alisema Dkt. Waane.

 “Maumivu ya kifua ni moja ya dalili kubwa za magonjwa ya moyo hususani shambulio la moyo, kwetu sisi ni muhimu kuwatambua wagonjwa wenye shambulio la moyo ili waweze kupata matibabu sahihi kutoka kwa wataalam wetu wabobezi wa magonjwa ya moyo,” alisema Dkt. Waane.

Aidha, Dkt. Waane alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo huduma mbalimbali zikiwemo huduma za upasuaji wa moyo kwa watu wazima na watoto, huduma za matibabu ya ndani kwa wagonjwa waliolazwa, huduma za matibabu ya upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab, huduma za kliniki kwa wagonjwa wa nje zimekuwa zikitolewa kwa watu wote wanaofika katika Taasisi hiyo.

“Huduma zetu za kliniki zinafanyika siku za Jumatatu hadi Jumamosi na huanza saa 12 asubuhi hadi saa 2 usiku kwa kuona wagonjwa kati ya mia tatu hadi mia nne kwa siku na kwa siku ya Jumamosi kliniki inaanza saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana”, alisema Dkt. Waane.

Mgonjwa anayepatiwa matibabu katika Taasisi hiyo, Grace Clement alisema yeye ni miongoni mwa wagonjwa ambao wamekua wakisumbuliwa na maumivu ya kifua kwa muda mrefu bila kuhisi kama maumivu hayo yanaendana na magonjwa ya moyo.

Grace alisema mwanzoni alihisi kifua kinamuuma kutokana na shughuli alizokuwa akifanya kila siku hivyo na pale aliposikia maumivu aliacha kufanya shughuli zake na kuamua kupumzika lakini maumivu hayakupungua na hivyo kuamua kufika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

“Nawashauri Watanzania wenzangu wanapojisikia maumivu ya kifua kufika kwa wataalam wa afya ili waweze kuchunguza maumivu hayo yanasababishwa na nini maana mimi nilifika hospitali nikachunguzwa na kufuata ushauri wa daktari wa kutumia dawa, kufanya mazoezi ili nipunguze uzito na leo naona maendeleo yangu kuwa mazuri,” alisema Grace.

Naye mgonjwa anayehudhuria kliniki za matibabu ya moyo JKCI, Salum Jabey alisema alikuwa na maumivu ya kifua baada ya kufanyiwa uchunguzi iligundulika kuwa baadhi ya mishipa yake ya damu imeziba.

“Nilikuwa nachoka sana nikitembea au nikiwa nafanya shughuli zangu za kila siku, kifua kinauma na mapigo ya moyo yanaenda kasi nikaenda hospitali ya Apolo walivyonichunguza wakanipa rufaa ya kuja hapa JKCI ambapo waligundua baadhi ya mishipa ya damu imeziba hivyo kunipatia matibabu.”

“Kwa sasa hivi dalili nilizokuwa nazo zimepungua kwa asilimia kubwa, nawashukuru wataalam wa afya wa hapa JKCI kwa kuendelea kutupatia matibabu, ushauri wangu kwa jamii wanapojisikia kuumwa wasiende kwa sangoma waende hospitali ambazo zipo kwa ajili yetu tuzitumie,”alisema Salum.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi