Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JITIHADA ZA SERIKALI KUKUZA KILIMO ZALETA NEEMA LINDI.
Mar 06, 2018
Na Msemaji Mkuu

Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma Wakulima Mkoani Lindi wamejipatia takribani bilioni 259 kwa kuuza mazao ya Biashara ikiwemo Korosho katika msimu uliopita baada ya Serikali kuweka msukumo na mazingira wezeshi katika uzalishaji na uuzaji mazao hayo. Akizungumza katika Kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari-MAELEZO, Mkuu wa mkoa huo Bw. Godfrey Zambi amesema kuwa dhamira ya mkoa huo ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya bishara ambapo kwa msimu uliopita jumla ya kilo milioni 75 za korosho zilizalishwa. “Mwaka 2017 Mkoa wa Lindi ulizalisha miche laki saba ya korosho na kuitawanya kwa wananchi wakati mwaka 2018 tumezalisha miche ya korosho milioni nne la laki tisa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza kilimo cha mazao ya biashara katika mkoa wetu” Akifafanua kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo Zambi amebainisha kuwa ujenzi wa gati katika bandari ya Lindi umeklamilika kwa asilimia 90 na kiasi cha shilingi bilioni 1 na milioni 800 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa gati hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa wananchi wa Mkoa huo. “Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na Afya bora Serikali imehakikisha kuwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni wakuridhisha na unaendana na mahitaji ya Mkoa wetu hivyo tunaipongeza Serikali kwa hatua hii” amesisitiza Bw. Zambi. Bw. Zambi ameongeza kuwa katika kuimarisha sekta ya afya, Mkoa huo umefanikiwa kupata watumishi watakaoziba pengo la wale walioondolewa katika utumishi wa umma kutokana na kuwa na vyeti  vya kughushi.   Akizungumzia ujenzi wa viwanda, Zambi amebainisha kuwa swala la kuanzisha viwanda 100 kila mkoa kwa upande wa Mkoa wa Lindi agizo hilo linatekelezwa  na kila Halmashauri  katika Mkoa huo. Kwa upande wa umeme alibainisha kuwa  Vijiji 180 vimeshanufaika na mradi wa REA na awamu ya tatu zaidi ya Vijiji 175 vitanufaika ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kufikisha nishati ya  Umeme katika Vijiji  vyote nchini. Aidha, kwa upande wa  upatikanaji wa huduma za maji  kwa wananchi wa Mkoa huo hasa Vijijini umefikia asilimia 53 ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na juihudi za kutafuta mzabuni  wa kujenga miundo mbinu ya kusambazia maji katika mkoa huo. Kipindi cha Tunatekeleza kinarushwa na Shirikika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO kikiwashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali ambapo awamu hii ni Wakuu wa Mikoa yote.    

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi