Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Jamii Yapaswa Kutokomeza Mila na Desturi Zinazowakandamiza Wanawake, Watoto Nchini.
Oct 27, 2018
Na Msemaji Mkuu

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof. Faustin Kamuzora ameiasa jamii kutokomeza mila na desturi potofu zinazokwamisha maendeleo ya wanawake na watoto sambamba na kuwapatia fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Wito huo ameutoa Oktoba 26, 2018 wakati akifungua mkutano wa Kamati Elekezi ya Taifa ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto uliohusisha Wizara 11 pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya wanawake na watoto nchini walipokutana mkoani Morogoro kujadili na kupitia Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.

“Jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupinga mila na desturi potofu zinazokandamiza makundi haya na badala yake kutumia muda mwingi katika kuzalisha mali na kujishughulisha katika masuala ya maendeleo ili kuondokana na umasikini na kujiletea maendeleo”.alisema Kamuzora

Aidha Kamuzora aliongezea kuwa, jamii inapaswa kuendelea kusaidia jitihada za Serikali katika kutokomeza mila na desturi potofu kwa kuunga mkono mipango mikakati iliyopo na kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya Haki na Usawa katika jamii.

“Tujitathimini na kuona namna bora ya kuondokana na mila na desturi zote zinazomkandamiza wanamke na mtoto ili kuendelea kusimamia zile zinazoiwezesha jamii kuwa na usawa na haki katika makundi yote bila kuwa na ubaguzi”

Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango Idara ya Maendeleo ya Jamii Bw.Atupele Mwambene alieleza kuwa, Serikali imejikita kuhakikisha inamaliza changamoto za wanawake na watoto kwa kuhakikisha Mpango Kazi huo unawawezesha katika maeneo nane ya kipaumbele ikiwemo; kutokomeza mila na desturi zilizopitwa na wakati, Uwezeshaji wa uchumi wa Kaya, kuhakikisha mazingira salama hususan mazingira ya umma na kuwa na malezi bora kuanzia ngazi ya familia.

Aliongezea kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendelea, hususan wanaoshirikiana katika masuala ya watoto na wanawake itaendelea kushirikiana ili kuwa na nguvu ya pamoja na kuhakikisha jamii inakuwa sehemu salama kwa makundi yote.

“Tumekutana pamoja ili kuhakikisha tunahuisha nguvu kwa pamoja ili kuhakikisha mila na desturi zinazochochea ukatili dhidi ya makundi haya unatokomezwa kwa kuwa na mipango inayotekelezeka.

Naye Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.John Njingu alieleza kuwa, jamii inapaswa kubadili mitazamo katika kupashana habari na kuvitumia vyombo vya habari kama nafasi pekee yenye mchango mkubwa katika kuifikia jamii kupitia elimu kwa umma juu ya utokomezaji wa vitendo vya ukatili katika makundi haya.

“watumiaji wa vyombo vya habari wawajibike na kuhakikisha taarifa zinazotolewa katika jamii zisiwe zenye athari kwa watoto na wanawake badala yake tutumia vyombo vya habari kwa matumizi yenye tija katika jamii zetu”.alisisitiza Dkt.Njingu

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi