[caption id="attachment_6230" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya James Foundation Bw. Leonard Manyama (kulia) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa tamko la kuunga mkono kauli ya Rais Magufuli kuhusu kutowarejesha shuleni wanafunzi wanaopata ujauzito, kushoto ni Mchungaji Bartholomew Sheygah toka Kanisa la Faith Community.
(Picha na: Eliphace Marwa)[/caption]
Na: Thobias Robert
Taasisi ya James Foundation imempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa tamko lake la kuzuia watoto wa kike watakaopata ujauzito wakiwa shuleni kuendela na masomo katika shule za msingi na sekondari nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Bw Leornard Manyama, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kuwa Taasisi ya James Foundation inaunga mkono tamko hilo la Rais Magufuli
“Lengo la Taasisi yetu kuja hapa ni kuunga mkono tamko la Rais wetu Magufuli la kutowarudisha shuleni wanafunzi wote wanaopata ujauzito wakiwa shule za msingi na sekondari za serikali” anasema Manyama.
Manyama alieleza kuwa, sababu kubwa iliyowafanya kumuunga mkono Mhe, Rais Magufuli ni pamoja na kulinda maadili ya taifa ambapo alisema kwamba Taifa lolote duniani ili liwe salama na kuendelea kustawi ni lazima lilinde maadili kwa gharama yoyote bila huruma.
Aliongeza kwa kusema kuwa, baadhi ya taasisi pamoja na wanasiasa wanaopinga tamko la Rais Magufuli, wanataka kuwafanya wanafunzi kutokuwa na msimamo, kujenga tabia zisizo na maadili ya kitanzania na kuliangamiza Taifa
Naye kiongozi wa Kanisa la Faith community Pentacoste church, Askofu Bartholomew Sheygah, amesema kuwa, jamii haina budi kulinda maadili ambayo yaliasisiwa na viongozi waliopita katika Taifa ili kuendeleza nidhamu na malezi bora kwa kizazi cha leo na kesho.
“Ni gharama kuweka msingi wa maadili ila kuubomoa unachukua muda mfupi. Wazazi, viongozi wa dini pamoja na walimu ni muhimu kushirikiana ili kuendeleza kizazi chenye maadili” anasema Askofu Sheygah.
Tamko la watoto wa kike waliopata ujauzito kutoendela na masomo lilitolewa na Mhe. Rais Magufuli alipokuwa akiwahutubia wananchi wakati wa ziara yake Mkoani Pwani ambapo alisema, ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi aliyepata ujauzito atakayerudi shuleni ili kuendelea na masomo baada ya kujifungua.