[caption id="attachment_28084" align="aligncenter" width="750"] Gari linaloonesha Mfano wa Mahakama inayotembea. Hivi karibuni Mahakama ya Tanzania itaanzisha Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ili kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani.[/caption]
Na: Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Watumishi wa Mahakama nchini kutoa huduma kwa kuzingatia Maadili, kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati pamoja na kuacha vitendo vya rushwa ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mhimili huo.
Akizindua wiki ya Sheria na Maonesho ya Elimu ya Sheria leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu alisema kuwa nguvu ya Mahakama ni imani ya wananchi na imani hiyo itaongezeka ikiwa hakuna rushwa, kuna maadili mema na kesi zitamalizika kwa wakati.
Jaji Mkuu pia amewataka wananchi kuacha kuilalamikia Mahakama na badala yake wachukue hatua kwa kuwataja watumishi wasiozingatia maadili kwa uongozi wa Mahakama.
[caption id="attachment_28086" align="aligncenter" width="750"] Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma akijiandaa kuanza Matembezi ya uzinduzi wa wiki ya Sheria leo jijini Dar es salaam. Kulia kwake ni mkewe akifuatiwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu na kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.[/caption]Aidha, amewashauri wananchi kujifunza na kuelewa taratibu za mashauri Mahakamani ili kurahisisha upatikanaji wa haki zao wanapozitafuta kwenye Mahakama mbalimbali nchini.
“Wananchi wengi wanakwenda kutafuta haki sehemu isiyohusika hivyo wanatakiwa kujifunza taratibu za Mahakama ili waweze kupata haki kwa wakati kwa kuwamuda mwingi unapotea kwa kutafuta haki mahali pasipostahili”, alisema Prof. Juma.
Alisema hivi sasa Mahakama inaingia kwenye matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano- TEHAMA hivyo matumizi haya yatamsaidia mwananchi kuweza kufahamu hatua zote za shauri lake lililopo Mahakamani.
Jaji Mkuu ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mnazi Mmoja ili kupata elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Mahakama na sekta ya sheria kwa ujumla.
[caption id="attachment_28089" align="aligncenter" width="750"] Maandamano ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yakiendelea[/caption]Alisema, katika maonesho hayo, wananchi watapata nafasi ya kujifunza juu ya usuluhishi nje ya Mahakama, Mahakama inayotembea (Mobile Courts) pamoja na changamoto za upatikanaji wa haki zikiwemo upungufu wa Watumishi, Miundombinu, pamoja na vifaa.
Akizungumzia taratibu wa usuluhishi wa kesi nje ya Mahakama (Mediation), Jaji Mkuu amesema wakati sasa umefika kwa wananchi kutumia utaratibu huo unaorahisisha upatikanaji wa haki na kuongeza kuwa Haki bora hupatikana kwa usuluhishi majumbani.
Aidha, kabla ya kuzindua wiki ya Sheria, Jaji Mkuu aliongoza Matembezi waliyowashirikisha watumishi wa Mahakama, wadau pamoja na wananchi kwa ujumla yaliyoanzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mpaka viwanja vya Mnazi Mmoja.
Matembezi hayo pia yalihudhuriwa na viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa wakati katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Sifuni Mchome pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju.