Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

IMF Yaunga Mkono Jitihada za Rais Magufuli Kupambana na Rushwa na Ukwepaji Kodi.
May 17, 2017

Na. Said Ameir

Shirika la Fedha Duniani (IMF) linaziunga mkono jitihada za Rais John Pombe Magufuli za kupambana na vitendo vya rushwa na ukwepaji wa kodi kwa kuwa hiyo ni sehemu ya kielelezo cha dhamira ya kweli ya Serikali yake ya kuleta maendeleo kwa faida ya wananchi wote.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dk. Tao Zhang amesema mjini Dar es Salaam leo kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi zinazofanya vizuri katika kukuza uchumi wake pamoja na kupata mafanikio katika sekta ya huduma za jamii ambayo ni matokeo ya kazi nzuri na sera madhubuti za uchumi.

“Ukuaji wa uchumi wenu umekuwa kwa kiwango cha wastani wa asilimia 7 katika miaka ya hivi karibuni na viashiria vya maendeleo katika sekta ya jamii ni vizuri kwa mfano kupungua kwa vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 60 na uandikishaji wa watoto elimu ya msingi umeongezeka kwa asilimia 36” Dk. Zhang alieleza.

   

Dk. Zhang aliongeza kuwa kutokana na mwenendo wa sasa wa ukuaji wa uchumi wake, Tanzania iko katika nafasi nzuri ya kupata mafanikio zaidi ikiwemo lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati kama ilivyoelezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2020.

“Kuna mambo mengi ambayo yanatoa fursa kwenu ikiwemo uanachama wenu katika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, raslimali ambazo zimo mbioni kupatikana katika miaka ya karibuni na rasilimali watu kubwa na iliyoelimika“, Dk. Zhang alieleza.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF, aliwaambia washiriki wa mhadhara huo kuwa kitu muhimu sasa kwa Tanzania ni kuendelea na usimamizi mzuri wa uchumi na kusimama katika kuchukua hatua kufungua fursa zake za maendeleo.

Dk. Zhang ameongeza kuwa, kama zilivyoweza kufanya nchi nyingine, anaamini Tanzania inaweza kufikia hatua hiyo, hivyo ameainisha maeneo matatu muhimu ambayo Tanzania ikiyafanyia kazi ipasavyo yataleta mabadiliko makubwa na kuipaisha nchi katika ngazi nyingine ya juu ya maendeleo.

 

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kuongeza uwekezaji kwa kushughulikia vikwazo vinavyozorotesha uwekezaji na kuongeza nafasi za ajira, kuchukua hatua madhubuti kuimarisha nafasi ya sekta binafsi katika uchumi na kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na kuhakikisha kuwa mafanikio yanayopatikana yanamfaidisha kila mwananchi kwa kupata fursa za elimu, afya na huduma za kifedha.

Dk Zhang, ambaye alikuwa akitoa mada kuhusu “Kufikia Mafanikio: Tanzania Kufikia Lengo la kuwa Nchi ya Kipato cha Kati” katika mhadhara uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu, mtaa wa Mirambo, amesema IFM iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha inafikia malengo yake ya maendeleo ikiwemo la kufikia nchi ya uchumi wa kiwango cha kati.

“Nchi yenu imepata mafanikio makubwa katika miaka ya karibuni na sisi (IMF) tuko pamoja nanyi kuhakikisha mnafikia malengo yetu ya maendeleo. Tumejiandaa kushirikiana nanyi kwa kusaidia ushauri wa kisera na kwa kuwajengea uwezo” Dk. Zhang alieleza.

Akizungumzia utenganamo wa kikanda, Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa IMF alieleza kuwa ametiwa moyo na kasi ya utengemano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuielezea kuwa moja kati ya ushirikiano wa kikanda unaokua haraka sana.

Mhadhara huo ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo makatibu wakuu, Mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa zilizopo nchini, wataalamu wa uchumi kutoka taasisi mbalimbali nchini wakiwemo wahadhiri na watafiti kutoka vyuo vya elimu ya juu na taasisi za utafiti pamoja na vyombo vya habari.

Mipangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi