Idadi ya mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 kwa mwaka 2020 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 1,310.34 kwa mwaka 2021.
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 30, 2022 Jijini Arusha na Mwenyekiti wa Kamati ya Ripoti ya Utafiti wa Watalii ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watalii Walioondoka nchini mwaka 2021.
Naibu Katibu Mkuu Mkomi amesema taarifa ya utafiti huo inaonesha kuwa Tanzania inazidi kufanya vizuri katika sekta ya utalii huku mapato yatokanayo na utalii yakiongezeka mwaka hadi mwaka.
Amesema mwaka mmoja baada ya mlipuko wa janga la UVIKO-19, idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 922,692 mwaka 2021 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 48.6.
Amezitaja sababu zilizochangia ongezeko la watalii hapa nchini mara baada ya mlipuko wa Janga la UVIKO-19 kuwa ni jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi.
Mkomi amesema, matokeo ya utafiti yanaonesha idadi kubwa ya watalii walikuja hapa nchini kwa ajili ya kutembelea hifadhi za wanyamapori na fukwe.
Utafiti huo umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Benki Kuu Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idara ya Uhamiaji, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirikisho la wawekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar ( ZATI).
Mkomi amesema takwimu za utafiti huo, zimepatikana kutokana na utafiti uliofanywa katika vituo vikubwa nane vya watalii, ikiwemo viwanja vya ndege vya kimataifa pamoja na maeneo ya njia za kuingilia na kutokea watalii.
Matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa idadi kubwa ya watalii wametokea nchi ya Ufaransa ikifuatiwa na Marekani, Kenya pamoja na Zambia
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Mkomi amesema matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku hapa nchini yaliongezeka kutoka Dola za Marekani 152 mwaka 2020 hadi kufikia dola za Kimarekani 199 mwaka 2021.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Utalii Wizara ya Maliasili na Utalii, Richie Wandwi amesema kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imejidhatiti kuwekeza nguvu katika utalii wa fukwe kwa vile ni aina ya utalii ambao unaonekana kupendwa na watalii wengi wanaoingia nchini.
Ameongeza kuwa, Wizara itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo baadhi ya watalii wamekutana nazo ili kuhakikisha idadi ya watalii inazidi kuongezeka na vivutio vilivyopo hapa nchini vinatangazwa kwa kasi zaidi katika Jumuia za Kimataifa.
Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa dunia ambapo idadi ya watalii duniani iliongezeka kwa takribani asilimia tano na kuchangia asilimia 6.8 ya mauzo ya nje, na kuzalisha ajira milioni 333.