Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Huduma za Posta Afrika Zaimarika, Mawaziri Wakutana Kimkakati
Aug 01, 2023
Huduma za Posta Afrika Zaimarika, Mawaziri Wakutana Kimkakati
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (katikati) akishiriki katika mkutano wa Jukwaa la Wasimamizi na Watoa Huduma wa Sekta ya Posta kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika jijini Arusha
Na Immaculate Makilika - MAELEZO

“Mamilioni ya wahudumu wa posta wasafirisha mabilioni ya barua na vifurushi kupitia maelfu kwa maelfu ya ofisi za posta duniani kote na hivyo kuzihudumia na kuziunganisha jamii kote duniani”, ameeleza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio  Guterres kupitia ujumbe wake mnamo 9 Oktoba 2021, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani.  

Katika kutimiza matarajio ya wananchi wa Afrika sambamba na kuendana na mabadiliko ya ukuaji wa teknolojia duniani, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza jana jijini Arusha, wakati akifungua Jukwaa la Wasimamizi na Watoa Huduma wa Sekta ya Posta kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika anasema kuwa wadau hao wamekutana nchini ili kujadiliana namna nzuri ya kuboresha  sekta hiyo kwa kuwa ni huduma muhimu barani Afrika inayohitaji kuboreshwa zaidi ili iendeelee kutoa huduma kulingana na mazingira ya sasa.

“Sekta ya Posta bado ni huduma muhimu katika utoaji wa huduma mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku na mtakumbuka kuwa hii ni sekta kongwe hivyo wamekutana kujadiliana ili kuona namna ambavyo Wasimamizi na Watoa Huduma za Posta wanaweza kuendelea kuboresha huduma hizi za posta. Huu ni mwendelezo wa mikutano kadhaa na kesho hapa Arusha kutakuwa na kikao cha Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Posta katika Bara la Afrika” anabainisha Waziri Nape.

Anaongeza kuwa uwepo wa Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Posta kutoka kutoka katika nchi za Liberia, Afrika Kusini, Uganda, Malawi na Tanzania ambao pia ni Wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) ambao wamekutana nchini Tanzania  kubadilishana mawazo na kujadiliana masuala yenye maslahi kuhusu Sekta ya Posta barani Afrika na ushirikiano wa kikanda.

“Huu ni uthibitisho kuwa dhamira yetu ya kukuza uhusiano thabiti na kutafuta msingi unaofaa katika kutekeleza malengo ya pamoja ya huduma zetu kwa wananchi wetu”, anasema Waziri Nape.

Wakati akifungua Mkutano wa 41 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika, Naibu wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew, aliyemwakilisha Waziri wake katika mkutano huo anasema kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) umefikia uamuzi wa kutumia mifumo ya kidijitali katika kutoa huduma za posta kulingana na mazingira ya sasa sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi katika nchi zao.

“Wanachama wa PAPU sasa  hawataki kuachana kwamba pengine Nigeria, Kenya au Uganda wako hatua fulani,  na ndio umuhimu sasa wa vikao kama hivi  tunataka tutembee  pamoja kama Afrika”, ameeleza Mhe. Kundo.

Ni dhahiri kuwa Afrika imedhamiria kuboresha sekta hiyo kongwe na hapa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt Khalid S. Mohamed wakati akifungua Mkutano huo wa 41 wa Baraza la Utawala la PAPU ametoa wito kwa wanachama wa PAPU kuwa na jitihada mbalimbali za kuboresha huduma za mawasiliano ikiwa katika maeneo ya mijini na vijijini.

“Nchi Wanachama wa PAPU mhakikishe mnaungana na kusaidiana katika kufikia malengo yenu na kamwe mipaka ya nchi isiwe kikwazo ili wananchi waweze kunufaika na uwepo na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika huduma za posta”, anabainisha Waziri Mohamed.

Naye, Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika, Dkt. Sifundo Chief Moyo anasema, Nchi Wanachama wa PAPU wachukue na kutekeleza  yale yote yaliyojadiliwa na kukubalika katika mikutano iliyolenga kutumia mifumo ya kidijitali ya utoaji huduma za posta kwa gharama nafuu sambamba na kuchangia uchumi wa nchi zao.

“Umoja huu unazidi kukua kwa kuboresha huduma mbalimbali za posta ikiwemo kushirikishana mbinu za mashirika ya posta kutokana na ukuaji wa teknolojia hususan teknolojia za simu na usafirishaji wa mizigo kupitia posta cargo” anaeleza Katibu Mkuu huyo.

Aidha, Tanzania imeendelea kuunga mkono jitihada za kuboresha Sekta ya Posta barani Afrika, ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza miradi ya kuboresha huduma hizi za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za posta za kidijitali kwa gharama nafuu.

Kadhalika, Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo anaeleza kuwa mikutano inayofanyika kuhusu kuboresha huduma za posta ni fursa ya kubadilishana uzoefu pamoja na kujadiliana changamoto za pamoja zinazoikumba sekta hiyo na namna ambavyo wataweza kuzitatua kwa pamoja na kusaidia kukuza maendeleo ya nchi za Afrika.

“Kama Tanzania tumepiga hatua ambazo nchi jirani wanajifunza na tayari ziko nchi mfano Kenya na  Zimbabwe ambazo tayari nina mwaliko wa kwenda kwao baada ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta wa Afrika hapa Arusha nitakutana nao kuwaeleza yale ambayo wanahitaji tuwasaidie” anabainisha Mbodo.

Umoja wa Posta Afrika (PAPU) umekuwa na mikutano kadhaa jijini Arusha nchini Tanzania inayolenga kujadiliana kuhusu mustakabali wa Sekta ya Mawasiliano hususan huduma za posta ikiwa ni maandalizi ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika linalotarajiwa kuzinduliwa mnamo Septemba 2, 2023 na  Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Fauka ya hayo, huenda huduma za posta barani Afrika zikawa na mtazamo mpya mara baada ya kuwepo kwa mikutano ya hivi karibuni inayowakutanisha watunga sera, watoa huduma na wasimamizi wa sekta ya posta ambao wanajadiliana kuhusu namna bora zaidi ya kutoa huduma za posta.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi