Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hospitali ya Wilaya Bukoba Kuanza Kutoa Huduma ya Mionzi Septemba, 2023
Aug 09, 2023
Hospitali ya Wilaya Bukoba Kuanza Kutoa Huduma ya Mionzi Septemba, 2023
Muonekano wa mashine ya mionzi iliyopo katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba
Na Mwandishi Wetu

Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imetakiwa kuanza kutoa huduma ya Mionzi na Upasuaji ifikapo  Septemba 1, 2023

Maelekezo  hayo yametolewa  na Mkurugenzi wa Idara ya Afya,  Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt.Ntuli Kapologwe  wakati wa kikao cha tahmini na ufuatiliaji kilichofanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba vijijini.

"Hospitali hii imejengwa mwaka 2017 na Serikali ya Awamu ya Sita imeshaleta Mashine za Mionzi na vifaa kwa ajili ya Upasuaji kwa hiyo hakuna sababu yeyote inayofanya huduma hizi zisiwepo hapa nawaelekeza kuanza kutoa huduma hiyo mara moja," amesisitiza Dkt.Kapologwe.

Amesema  hospitali hiyo imegharimu shilingi bilioni 3.1, hivyo amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha huduma hizo zinaanza kutolewa ifikapo Septemba 1, 2023.

"Naelekeza, ifikapo mwezi Septemba mwaka huu  huduma hizi ziwe zimeanza na unipe taarifa. Nataka ikifika tarehe hiyo nione picha ukiwa umemshika mtoto aliyezaliwa katika chumba hiki cha upasuaji,” amesisitiza Dkt.Kapologwe.

Vilevile,  Dkt.Kapologwe amesisitiza uwajibikaji wa kiwango cha juu kwa wafanyakazi wote wa sekta ya Afya nchini ili kuweza kutimiza lengo kuu la kutoa huduma bora za afya kwa  wananchi.

"Serikali imeajiri watumishi wapya  wa Afya zaidi ya 24,000 na wengi wenu ni vijana hivyo nawasisitiza kutumia ujuzi wenu vizuri ili tuone matokeo chanya,” amesema Dkt.Kapologwe.

Aidha, amemtaka  Mganga Mkuu wa wilaya na Mkoa  kuwajengea  uwezo watumishi wapya ili waweze kuendana na Mazingira.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo hayo na kusema kuwa hadi ifikapo Septemba shughuli  za upasuaji na mionzi zitakuwa zimeanza kutolewa.

Timu ya tathmini , ufuatiliaji na  usimamizi shirikishi kutoka TAMISEMI ipo katika ziara ya kukagua miradi na ubora wa huduma za chanjo, Lishe na Ustawi wa Jamii Mkoani Kagera.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi