Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Ibenzi Ernest amesema kuwa hospitali hiyo ina zaidi ya miaka 103 tangu kuanzishwa kwake lakini haijachoka kutokana na ubora wa huduma za afya zinazoendelea kutolewa na hospitali hiyo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hospitali hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wake kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 leo Agosti 9, 2023 katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma.
Dkt. Ernest ameeleza kuwa, hospitali hiyo inaendelea kuhudumia wagonjwa wengi ambapo kwa sasa kwa siku wagonjwa wanaokuja na kuondoka ni takriban 1,500 na wanaolazwa ni kati ya 250 hadi 350 ambapo kutokana na wingi wa wagonjwa, hospitali ilifanya ugatuzi wa huduma kwa kufungua mageti matatu ili kupunguza msongamano wa matibabu ambapo kila eneo limewekewa huduma zote zinazohitajika.
“Hospitali hii ilianzishwa mwaka 1920 ikiwa ni kituo kidogo cha kutolea Huduma za Afya, ni ya muda mrefu sana lakini imeendelea kuwa na nguvu kuliko kule ilipotoka kwani kwa sasa kuna dawa za kutosha, hali nzuri ya majengo na mitambo na inaboreka zaidi kupitia utekelezaji wa majukumu ikiwemo; utoaji huduma za tiba na kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, utoaji elimu ya afya na kufanya tafiti na mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na watarajali wa fani mbalimbali,” amesema Dkt. Ernest.
Amefafanua kuwa, mwelekeo wa hospitali hiyo ni kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi ambapo kipaumbele kikubwa ni kuponya Watanzania wanaofika katika hospitali hiyo wakiwa wagonjwa, tena wapate tiba kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi.
Ametaja baadhi ya mafanikio kuwa ni kuongoza katika utoaji huduma kwa wagonjwa waliovunjika mifupa, kujenga jengo la watoto ili kupunguza mbanano wodini, kuongeza uwezo wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) kutoka kuhudumia wagonjwa Watatu hadi 38 na kuweka vitanda 32 vya wagonjwa hao katika jengo la wagonjwa wa dharura, kuongezeka kwa vifaa tiba ikiwemo mashine za X-rays, CT Scan na Ultra Sound, kukarabati miundombinu na kurekebisha maeneo kuendana na uhalisia wa Makao Makuu.
Vilevile, mafanikio mengine ni upatikanaji wa kutosha wa dawa na hewa tiba (oxygen), utatuzi wa changamoto ya harufu mbaya hospitalini hapo kwa kupata mitambo ya kumeng'enya uchafu na kuubadili kuwa gesi ya kupikia pamoja na uwepo wa mitambo ya umeme wa jua ambayo inatumika katika jengo la mama na mtoto.