Na Immaculate Makilika MAELEZO
Serikali ilitoa Shilingi bilioni 1.1 kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa na Shilingi milioni 400 zilizotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kununua na kusimika mtambo wa kuzalishia hewa tiba, kununua mitungi 560 na gari la kusambazia hewa tiba hiyo katika hospitali mbalimbali wakati wa mlipuko wa UVIKO-19.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma wakati akieleza kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya Hospitali hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika amesema Mtambo huu una uwezo wa kuzalisha mitungi 400 ndani ya masaa 24.
Tangu mtambo uzinduliwe, Julai 1, 2022, jumla ya mitungi 13,467 imeshazalishwa ambapo mitungi 10,962 imetumiwa hospitalini hapa na mitungi 2,505 imesambazwa kwenye Hospitali zenye mahitaji.
Katika kipindi cha UVIKO-19, Hospitali hii ilikuwa ikitumia zaidi ya mitungi 200 kwa siku idadi ambayo ilikuwa ikitumika katika hospitali hiyo kwa mwezi mzima kabla ya mlipuko wa ugonjwa huo, hivyo uwekezaji huu ni wa tija sana. Amebainisha Dkt. Chandika.
Ameendelea kwa kufafanua kuwa uzalishaji wa mitungi hiyo Hospitalini hapo ndani ya kipindi kifupi, umeokoa zaidi ya shilingi milioni 500 na imeongeza mapato ya ndani ya hospitali kwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 75 ambazo Hospitali nyingine zinachangia kwa kupelekewa huduma hiyo.
Katika hatua nyingine, Hospitali ya Benjamin Mkapa ilipata mgao wa fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) wa jumla ya shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambazo zilitumika kuboresha huduma za dharura.
Kitengo cha huduma hizo kimeboreshwa ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vitanda kutoka vitanda sita hadi 22, kuwepo kwa Digital X-RAY na magari ya kubebea wagonjwa wa dharula mawili yanatarajiwa kupokelewa pamoja na kufungwa vifaa vya kutolea huduma za tiba mtandao na vifaa vya maabara.