Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hospitali ya Apollo Kujengwa Nchini
Oct 13, 2023
Hospitali ya Apollo Kujengwa Nchini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine.
Na Mwandishi wetu- New Delhi, India

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara ya Afya kufufua mchakato wa mazungumzo wa ujenzi wa Hospitali ya Apollo nchini na kuelekeza Mfuko wa Hifadhi za Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kuona njia watakazoweza kushirikiana kutekeleza ujenzi wa Hospitali hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Rais Samia amesema hayo Oktoba 11, 2023 kufuatia mazungumzo baina yake na Mwenyekiti mwanzilishi wa Hospitali za Apollo nchini India, Dkt. Prathap Reddy kwa njia ya mtandao ambapo mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu na Mkurugenzi wa Hospitali za Apollo, Bi. Sangita Reddy.

Kwa upande wake Dkt. Prathap Reddy ameahidi kuanza utekelezaji wa mradi wa hospitali hiyo Jijini Dar es Salaam kwa awamu na utekelezaji wake utaanza mara moja endapo serikali itakamilisha hatua zote zinazotakiwa katika mchakato wa ujenzi huo.

Aidha, Dkt. Reddy amepongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Rais Samia katika kuboresha huduma za afya nchini na kuimarisha huduma za tiba za kibingwa na bobezi pamoja na  kuanzisha huduma za tiba kwa njia ya mtandao.

Dkt. Reddy amesema kuwa huduma za tiba mtandao zitaleta ufanisi wa huduma kwa njia ya mtandao (TeleEmergency) na kuleta ufanisi wa huduma kuanzia kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi (TeleICU) na idara za dharura katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

Mtandao wa hospitali wa Apollo una hospitali zaidi ya 73 duniani, tangu kuanzishwa kwake imeshatoa huduma kwa zaidi ya wagonjwa milioni 150 kutoka katika Mataifa zaidi ya 140 duniani, ujenzi wa hospitali hiyo hapa nchini ni juhudi za dhati za Rais Samia katika kuboresha huduma za kibingwa na bobezi kupatikana karibu zaidi kwa Watanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi