Na. Edward Kondela
Serikali imesema ugonjwa wa Homa ya Mgunda usiwe kikwazo cha Watanzania kutokula nyama na kwamba asilimia tisini ya nyama inayopitia kwenye machinjio rasmi iko salama.
Akizungumza leo jijini Dodoma kupitia vyombo mbalimbali vya habari, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga amesema, nyama ya mnyama anayechinjwa kwenye machinjio rasmi huwa inakaguliwa na mtaalamu wa mifugo wa Serikali kabla ya kwenda sokoni ili kuepusha madhara yoyote kwa binadamu.
Prof. Nonga amebainisha kuwa kutokana na utafiti uliofanywa umebaini kuwa mnyama ambaye ameathirika na vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda akitolea mfano wa ng’ombe, nyama yake inakuwa na rangi ya njano hivyo ni rahisi kwa mtaalam wa mifugo kubaini nyama hiyo machinjioni na kutoruhusu kupelekwa sokoni.
“Kuchinja mifugo kwenye machinjio na nyama ikaguliwe na daktari au mtaalamu wa mifugo wa Serikali kwa kuwa tushaona ng’ombe akipata shida ya Homa ya Mgunda, nyama yake inakuwa na rangi ya njano hivyo mtaalam atagundua kuwa haifai kwa matumizi ya binadamu, hivyo watanzania watakuwa salama.” Amesema Prof. Nonga.
Ameongeza kuwa njia nyingine ya watanzania kujikinga na ugonjwa wa Homa ya Mgunda ni kuhakikisha nyama inapikwa vyema na kuiva ili kuua vimelea vya ugonjwa huo ambavyo vinaishi kwenye majimaji ya mnyama ambaye ameathirika, ukiwemo mkojo na kinyesi chake.
Aidha, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga amewataka watanzania kutokula nyama ya wanyama wasio rasmi kwenye chakula akiwemo panya kwa kuwa amebainika kuwa ni moja ya wanyama ambao wanahusishwa kwa kiasi kikubwa kubeba vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda na magonjwa mengine.
Amefafanua kuwa ulaji wa nyama ni muhimu katika mwili wa binadamu kwa kuwa ni chanzo cha Protein katika daraja la kwanza ikiwa ni pamoja na kinga mwilini, hivyo watanzania wanatakiwa kula nyama iliyo rasmi katika kundi la chakula, kununua nyama iliyokaguliwa kwenye machinjio rasmi pamoja na kuipika nyama hiyo vyema na kuiva ili kuua vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda pamoja na magonjwa mengine.
Pia, amewaasa wafugaji kuhakikisha wanachanja mifugo yao dhidi ya magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa Homa ya Mgunda ambao umekuwepo kwa siku nyingi lakini umeanza kuonesha athari kwa binadamu.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania, Dkt. Daniel Mushi amewatahadharisha watanzania wanaokula nyama kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya starehe kuhakikisha nyama imechomwa na kukauka vizuri na kutokuwa na damu kwa kuwa ikipikwa vizuri hakuna sababu ya kuogopa ugonjwa wa Homa ya Mgunda kwa sababu vimelea vyake vinakufa kwenye mapishi yanayofikia nyuzi joto sabini (70).
Dkt. Mushi amewaasa pia watanzania kununua nyama kwenye maduka yaliyosajiliwa na kukaguliwa ambapo nyama iliyokaguliwa inakuwa na mhuri kwenye mguu wa nyuma wa mnyama na kuwataka kuacha kula nyama kutoka kwenye machinjio yasiyo rasmi yasiyoeleweka au nyama inayopatikana mitaani kwa bei nafuu kwa kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu.
Ameongeza kuwa ni wajibu kwa watoa huduma kwenye maduka ya nyama kutakiwa kupimwa afya zao kila baada ya miezi sita ili wasiwe chanzo cha maradhi mengine kwa walaji wa nyama wanazouza.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Bodi ya Nyama Tanzania zimelazimika kutoa taarifa juu ya ugonjwa wa Homa ya Mgunda kwa nyama inayopatikana kutoka kwenye mifugo hapa nchini, kutokana na uwepo wa baadhi ya taarifa zisizo sahihi juu ya uwepo wa ugonjwa huo na ulaji wa nyama.