Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hoima-Tanga: Ni Safari ya Kihistoria, Tunatekeleza
Aug 05, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_8482" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wakifunua kitambaa kuashiria kuwekwa kwa jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Tanga Nchini Tanzania, wanaoshuhudia Kulia ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Nishati na Madini Mhe. Medard Kalemani na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Kushoto ni Waziri wa Nishati wa Uganda Mhe. Irene Muloni[/caption] [caption id="attachment_8477" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpa mkono Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni baada ya kumaliza kuhutubia katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Tanga Nchini Tanzania.[/caption]

Na Dkt. Hassan Abbasi

Miaka mitano iliyopita maisha ya wakazi 4,000 hivi wa rasi ya Chongoleani nje kidogo ya jiji la Tanga, huenda yalikuwa kama maisha ya wakazi wengine wa Pwani ya uvuvi na uvunaji wa chumvi.

Wakati maisha ya wakazi wa Chongoleani yakiendelea kuwa hivyo, kwa sadfa tu, hali ni kama hiyo kwa ndugu zao umbali wa takribani kilometa 1500 katika ukanda wa Pwani ya Ziwa Albert huko Uganda.

Kisha jambo moja linatokea: ugunduzi wa mafuta katika Ziwa Albert sasa unakwenda kuyabadili maisha yao, uchumi wao na historia yao.

Ni mradi unaofungua historia kwa Uganda kupata bomba la kwanza lakini ni historia nyingine kwa Tanzania katika miundombinu ya mabomba, baada ya lile la mafuta la Tanzania-Zambia na la gesi la Mtwara-Dar es Salaam.

[caption id="attachment_8481" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Tanga Nchini Tanzania ambapo aliwataka wananchi wa nchi za Uganda na Tanzania kuutumia mradi huu kwa manufaa ya nchi hizi mbili.[/caption]

Lakini pia ni bomba linaloendelea kuiweka Tanzania na Uganda katika nafasi ya kimkakati zaidi kiuchumi na kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani.

Kwa viongozi wakuu wote, akiwemo Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan na hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, walipopata fursa adhimu ya salaam katika uzinduzi huo, hawakusita kuonesha bashasha yao na sura ya kuwapa matumaini wana Chongoleani na wenzao wa Hoima.

[caption id="attachment_8476" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni akiongea wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima Nchini Uganda hadi Tanga Nchini Tanzania ambapo alisema mradi huu uwe chachu ya kuimarisha uchumi ili kuwa na jumuiya imara ya Afrika Mashariki.[/caption]

Kwa furaha zaidi Mama Samia alihitimisha salaam zake kwa kusisitiza pia msisitizo wetu wa kila siku kuwa katika maendeleo hakuna siasa na ahadi kwa wananchi ni moja tu: “TUNATEKELEZA.”

Ni uzinduzi uliojaa historia, kumbukizi ya undugu na kushuhudiwa mara kadhaa wakitajwa viongozi wakuu waasisi wa pande hizi mbili kama Mwalimu Nyerere na Mzee Obote.  

Haikushangaza kuona katika hotuba yake ya utangulizi, akitumia lugha adhimu ya Kiswahili mara kadhaa, Rais Yoweri Museveni alikumbusha mengi ya historia na kuuita uzinduzi huo kuwa: “ni uthibitisho wa undugu wa Watanzania na Waganda.”

Shujaa wa mradi huo akatajwa kutoka kinywani mwa Rais Museveni alipotoa siri akisema: “Nafuu kubwa za kodi tulizopewa na Rais Magufuli kama vile kodi ya ongezeko la thamani na nyingine nyingi ni uamuzi wa kukumbukwa.”

Huenda waliokuwepo pia walishangazwa na bashasha nyingi zilizopamba uzinduzi huo hasa kwa viongozi wakuu. Ipo sababu na sadfa nyingine muhimu kuhusu kisa cha Chongoleani na Hoima.

Nayo ni: licha ya nchi hizi kung’aa katika ripoti ya Quantum Lab taasisi ya Uingereza kwa Tanzania kuwa ya kwanza kuvutia wawekezaji na Uganda kuwa ya pili katika EAC, viongozi wetu hawa wana uzalendo unaotokana na kulelewa vyema.  

Marais vinara wa mradi huu Mzee Museveni na Mzee Magufuli wote ni zao la malezi mema kutoka Chuo Kikuu mashuhuri katika ukanda huu na duniani cha Dar es Salaam (UDSM).

Viongozi hawa pia pale UDSM wamesoma taaluma zilizokuwa muhimu kuamua mradi huu. Wakati Museveni alianzia sheria kisha akahamia darasa la sayansi ya siasa, Mzee Magufuli alisoma sayansi ya kemia.

Sayansi ya siasa na sayansi ya kemia zilikuwa muhimu katika kuamua kwa nini mradi huu upitie Tanzania na si kwingineko.

Ndio maana naye aliposimama kuhutubia katika mradi huo, Rais Magufuli, alishadidisha dhana hii ya sayansi za siasa na kemia kusaidia kufikiwa mradi huu na akatoa siri aliposema:

“Pamoja na Mzee Museveni kuwa ndugu wa Watanzania lakini katika mradi huu alifuatwafuatwa sana kutaka mradi usije Tanzania. Lakini namshukuru kwa kusimamia udugu huo. Na sisi ilibidi kuchomekea baadhi ya mambo ili mradi uje kwetu.”

“Haijapata kutokea,” ndio neno la kuhitimisha la Rais Magufuli alipokuwa akieleza faida za mradi huo kwa Watanzania akionesha namna uzinduzi huo tu tayari ulivyoifanya Chongoleani na Tanga kufurika na kung’aa.

Kibwagizo cha “Ishi na Mimi” kutoka kwa wasanii nyota wa wakiongozwa na Mrisho Mpoto “Mjomba” kilitosha kuwathibitishia viongozi “wanasayansi” hao kuwa hawakukosea kufikia mradi huu na kilikuwa ukumbusho tosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuishi salama na mradi huo, kuutunza na kuuenzi.

Wakati “Ishi na Mimi” ikihamasisha mapenzi kwa mradi huo, huenda uzinduzi wa Chongoleani ukawa changamoto kwa wasanii wenzao wa kundi la “Wagosi wa Kaya” ambao huenda baada ya awali kuimba wakihoji Tanga kunani mbona kila kitu kimekufa sasa watalazimika kupitia upya mashairi yao.

Na mwishowe uzindushi wa bomba Chongoleani na kibwagizo cha “Ishi na Mimi” vitabaki pia kuwa jambo la kukumbukwa, na kama kutakuwa na wakati murua wa kumbukizi hii ni pale somo kutoka wimbo huo lilivyomfanya Mhe. Rais kuwakutanisha viongozi vijana wawili Ruge Mutahaba na Paul Makonda na wakapeana mikono.

Hivi ndivyo safari ya kihistoria na iliyosheheni bashasha ilivyoanza Pwani ya Chongoleani, safari ya kazi, na safari ya kilometa 1,445 itakayoishia katika Pwani ya Ziwa Albert.

Ni safari itakayopita katika nyakati za kiza, mwanga, baridi, joto na jua kali, milima na mabonde lakini kama walivyosema wasanii wetu na walivyosisitiza Marais wetu ni safari tunayopaswa kuishi nayo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi