Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

HESLB Kufanya Kazi kwa Bidii, Maarifa na Nidhamu Katika Utoaji Huduma
Aug 19, 2020
Na Msemaji Mkuu

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru akizungumza na baadhi ya Viongozi kutoka Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU) aliokutana nao jana Jumanne (Agosti 17, 2020) Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Makamu Mkuu wa Chuo cha (MUCOs) Prof Alfred Sife.

Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kufanya kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu kwa wateja wake ili kukidhi matarajio ya utoaji huduma bora kwa wanafunzi waombaji na warejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu nchini.

Akizingumza jana Jumanne (Agosti 18, 2020) Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya waliohamia HESLB katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Badru alisema kila mtumishi ndani ya HESLB anapaswa kutoa huduma bora kwa wateja kwani ndiyo wajibu wa msingi wa mtumishi wa umma.

Badru alisema wateja ndio msingi mkuu wa uwepo wa taasisi yoyote ya umma, hivyo ni wajibu wa watumishi wa HESLB kuhakikisha inawadumia vyema wateja wote wanaofika katika ofisini hapo, ambapo sehemu kubwa ni pamoja na wanafunzi waombaji mikopo na waliokuwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru (katikati) akizungumza na watumishi wapya waliohamia Ofisi hiyo kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali wakati wa mafunzo elekezi yaliyotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa watumishi hao jana Jumanne Agosti 17, 2020 Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) Mariam Muhenga pamoja na Viongozi waandamizi wa HESLB.

“Wateja wetu ndio watu wanaotuweka mjini, hawa ndio msingi wa uwepo wetu, tunapaswa kuwahudumia vyema, tusiwe kikwazo kwa wateja kupata huduma, tufanye kazi kwa nidhamu katika kutekeleza majukumu katika maeneo yetu ya kazi’’ alisema Badru.

Akifafanua zaidi, Badru alisema ni wajibu wa watumishi hao wapya kujituma katika maeneo yao ya kazi na kuwapongeza kuhamia HESLB kwa kuwa taasisi hiyo inatumia mifumo mbalimbali ya kupima walionao katika kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa utaratibu ikiwemo kutumia Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).

Watumishi wapya waliohamia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi ya Elimu ya Juu (HESLB) kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Rose Marlaw na Paul Machimo wakisililiza mada mbalimbali zilizotolewa wakati wa mafunzo elekezi yaliyokuwa yakitolewa na mtoa mada kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) jana Jumanne Agosti 17, 2020 Jijini Dar es Salaam.

Aidha Badru aliwaka watumishi wa Ofisi hiyo kutunza rasilimali za umma ikiwemo vifaa na vitendea kazi vinavyotolewa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya ofisi hiyo na kuongeza kuwa watumishi wote kuendelea kushirikiana katika usimamizi wa rasilimali hizo ili ziwe na matumizi endelevu kwa manufaa ya taasisi hiyo.

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Mariam Muhenga alisema utoaji wa huduma bora kwa wateja ni moja ya misingi ya kanuni za maadili ya utumishi wa umma, hivyo ni wajibu wa mtumishi wa HESLB kuhakikisha kuwa anasimamia kanuni hizo ili kuleta tija katika maeneo ya kazi.

Aliongeza kuwa mtumishi wa umma ni kioo katika jamii, hivyo anapaswa kuzingatia kuwa mfano wa kutazamwa katika taswira chanya wakati wote anapokuwa anatekeleza wajibu wake katika kutoa huduma kwa wateja.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi