Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa jumla hekta 296,881 za maeneo ya hifadhi kwa Wananchi ikiwa ni hatua ya kutatua migogoro katika maeneo ya hifadhi hizo.
Akieleza kwa Waandishi wa Habari leo katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Prof. Dos Santos Silayo amesema hatua hiyo inalenga kutatua migogoro na kuwawezesha Wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na kujenga makazi.
“Wakala unaendelea kutoa elimu ya uhifadhi na usimamizi wa misitu kwa jamii sambamba na kuimarisha mipaka kwa kuisafisha, kuweka vigingi na mabango ili kuzuia uvamizi katika maeneo ya hifadhi,” ameongeza Prof. Silayo.
Akizungumza kuhusu usimamizi wa mikoko, Prof. Silayo amesema kuwa, Tanzania ina eneo la mikoko linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 158,100 hivyo wakala umeendelea kuhifadhi maeneo hayo kwa kupanda miche 70,346 kwenye eneo la hekta 31 katika Delta ya Rufiji na mwambao wa Wilaya ya Kinondoni.
Aidha, Prof. Silayo amebainisha kuwa, katika jitihada za kukabiliana na majanga ya moto kwenye hifadhi za misitu, Wakala umesafisha mipaka na njia za moto zenye urefu wa kilomita 5,416.
“Wananchi zaidi ya 19,170 kutoka vijiji 348 walipatiwa elimu ya athari za moto na mbinu za kukabiliana na matukio ya moto, hivyo kwa upande mwingine, vikosi vya kukabiliana na matukio ya moto vyenye jumla ya watu 365 viliimarishwa kwa kupewa mafunzo sambamba na kukarabati minara 21 ya kuangalizia moto katika mashamba ya miti,” ameongeza Prof. Silayo.
Wakala uliimarisha matumizi ya mitambo ya kuzimia moto na mfumo wa satelite wa kubaini matukio ya moto mapema ili kuukabili kabla ya kuenea na kusababisha madhara zaidi.