Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Halmashauri ya Kalambo Yazindua Miongozo ya Uboreshaji Elimu
Oct 05, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Afisa Habari - Kalambo Rukwa


Halmashauri ya Kalambo mkoani Rukwa imezindua rasmi miongozo ya uboreshaji wa elimu ya  msingi na sekondari utakaosaidia kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari.

Awali akiongea kupitia uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Ndg. Wambura Sanday alisema miongozo inalenga kutoa chakula mashuleni, kuimarisha mafunzo endelevu kazini kwa walimu, kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kubaini changamoto na kuzitatua kwa wakati.

Alisema Halmashauri ya Kalambo imepokea vitabu vya mwongozo kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu msingi toleo la Julai 2022 ambavyo vilizinduliwa na Mhe, Queen Sendiga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Septemba 12, 2022 .

‘’Baada ya uzinduzi huo, Mhe. Mkuu wa Mkoa aliagiza vitabu hivyo vikazinduliwe na kugawiwa kwa walimu mashuleni ili lengo la serikali liweze kufikiwa", alisema Wambura

Mapema akiongea kupitia kikao hicho, Mkuu wa Wilaya Mhe. Tano Mwela aliwataka walimu kuitumia miongozo hiyo katika kusaidia kuimarisha umoja baina yao na wazazi mashuleni kwa kutoa mitihani ya mara kwa mara kwa wanafunzi.

Alisema miongozo hiyo itasaidia kuimarisha umoja wa walimu na wazazi mashuleni, kutoa mitihani ya mara kwa mara kwa wanafunzi, walimu kufundisha kwa kutumia mbinu shirikishi na kudhibiti utoro wa walimu na wanafunzi .

‘’Ndugu washiriki ni mategemeo yangu kuwa baada ya uzinduzi huu mtaanza kuitumia miongozo hii na mtaandaa utaratibu wa namna bora ya kuwashirikisha wadau wengine wa elimu katika ngazi zenu za uongozi ili iwe rasmi katika utekelezaji’’, alisema Mhe. Tano Mwela Mkuu wa Wilaya ya Kalambo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi