Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe amesema hakuna sababu ya kuendelea kukiuka haki za binadamu na ukatili kwa wanawake na wasichana kutokana na mila zenye madhara.
Mhe. Riziki ameyasema hayo wakati akihitimisha mkutano wa pili wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya kutokomeza ukeketaji uliofanyika jijini Dar Es Salaam Oktoba 9-11, 2023.
Amesema mikakati madhubuti iliyowekwa katika maazimio ya mkutano huo yataleta mabadiliko kwa kizazi kijacho katika kupambana na Ukeketaji.
"Jambo hili si tu linakiuka haki ya msingi ya wanawake na wasichana bali pia ni ukatili mkubwa ambao sote tunakubaliana kwamba haukubaliki", amesema Waziri Riziki
Ameongeza kwamba, teknolojia itumike kuwakutanisha wadau wote na kubadilishana mawazo ya kutekeleza maazimio waliyojiwekea ili kutokomeza kabisa ukeketaji Afrika na duniani kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Toufiq akizungumza katika mkutano huo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha haki za wanawake na watoto zinalindwa kwa kukubali Programu za kutokomeza ukeketaji zisimamiwe.
"Hapa Tanzania juhudi mbalimbali zimefanyika tangu mwaka 1990 hatimaye Sheria ya kupinga ukeketaji ilitungwa mwaka 1998 na katika kuendeleza mapambano, Serikali imeandaa mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukeketaji pamoja sheria ya mtoto"
Nao baadhi ya washiriki wa mkutano huo wamesema makubaliano yaliyopatikana kwa pamoja watayafikisha katika Mamlaka za nchi zao ili hatua ziweze kuchukulua katika kupambana na kutokomeza vitendo vya Ukeketaji Afrika.