Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hakuna Aliye Juu ya Sheria – Rais Samia
Sep 11, 2023
Hakuna Aliye Juu ya Sheria – Rais Samia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wadau wa Demokrasia kabla ya kufungua Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Hali ya Siasa nchini. Mkutano huo umefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Septemba, 2023.
Na Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa falsafa zake za maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na ujenzi mpya amezichukua kama msingi unaomuongoza katika kuongoza nchi ili isonge mbele kama Taifa kwa pamoja.

 

Amesema hayo  leo jijini Dar es salaam wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa unaoshirikisha Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa kwa lengo la Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Kujadili Hali ya Siasa nchini.

 

Mhe. Rais Samia amesema kuwa tayari Serikali imeshaanza kutelekeleza mapendekezo ya kikosi kazi ikiwemo kuruhusu kufanyika mikutano ya hadhara ambapo kwa sasa mikutano hiyo inafanyika sehemu mbalimbali nchini.

 

“Hatukutoa fursa ya mikutano ya hadhara ili watu kuvunja sheria, tumieni fursa hii kujenga Sera zenu kwa wananchi na si vinginevyo. Hakuna aliye juu ya sheria, atakaye fanya kosa atachukuliwa hatua za kisheria, kila mtu adumishe amani, umoja na mshikamano wa kitaifa”, ameeleza Rais Samia.

 

Ameongeza kuwa kuna uhuru wa kutoa maoni lakini una mipaka yake kisheria na kibinadamu na kuwa marekebisho ya Katiba yameanza kufanyiwa kazi, si mali ya Vyama vya Siasa bali ni mali ya Watanzania wote.

 

“Hatutakurupuka katika hili, tutaenda taratibu ili kuweka kila kitu sawa ikiwemo kutoa elimu kwa Watanzania ili kila mtu atoe maoni yake ya nini kibadilike, demokrasia sio matusi, demokrasia ni kutoa maoni, tusiitumie vibaya. Vyama vya Siasa nawakumbusha misingi yetu kufuatwa ambayo ni pamoja na kuheshimu maazimio yetu, kuheshimu sheria za Serikali, kuheshimiana”, amesisitiza Rais Samia.

 

Naye, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuwa Ofisi yake na Ofisi ya Makamu wa Rais Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mawaziri wa nchi wa ofisi hizo wameendelea kuratibu hatua kwa hatua hadi kuunda vikosi kazi ambavyo vimeendelea kufanya jukumu la kuratibu shughuli za kisisasa na hatimae kuifikia hatua ya kuwa na mpango mkakati wa namna ya kwenda ili kuimraisha mwenendo wa vyama nchini.

 

“Mheshimiwa Rais tangu ulipoingia madarakani kwa dhamira yako na kwa nia njema yako uliona upo umuhimu wa vyama vyetu vya siasa kukaa meza moja kuzungumza lakini pia kupitia changamoto zinazozikabili kwa maslahi ya taifa. Leo hii tunakutana hapa ikiwa ni kikao cha kutathimini utekelezajii wa mapendekezo yaliyochakatwa na vikosi kazi vyetu na pia kujadili hali ya siasa nchini”, Amebainisha Waziri Mkuu Majaliwa.

 

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema kuwa mikutano hiyo inasaidia kufungua fursa ambazo zimeminywa za Wadau kukaa kwa pamoja na kueleza changamoto zinazowakabili.

 

“Mkutano huu umefurika kwa kuwa hatujawahi kuwa na mikutano ya aina hii ambayo inatusaidia kuondoa zile nyufa zinazokuwepo”, amesema Jaji Mutungi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi