Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

GST Moyo wa Sekta ya Madini - Mavunde
Sep 05, 2023
GST Moyo wa Sekta ya Madini - Mavunde
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa GST jijini Dodoma, ikiwa ni kikao chake cha kwanza baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.
Na Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema Taasisi ya Jiolojia na Ufafiti wa Madini Tanzania (GST) ndiyo Moyo wa Sekta ya Madini na ni Taasisi inayotegemewa na Wizara ya Madini na Sekta ambata kama Sekta ya Maji, Kilimo na Ujenzi.

Mhe. Mavunde ameyasema hayo Septemba 4, 2023 wakati wa kikao na watumishi wa GST jijini Dodoma, ikiwa ni kikao chake cha kwanza baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.

Amesema kuwa GST inafanya tafiti mbalimbali na kupelekea kugundua migodi ya wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo, ameahidi kuipa kipaumbele taasisi hiyo baada ya kuonekana ina mchango mkubwa kwenye sekta hiyo.

"Kulingana na historia GST ni kinara wa utoaji wa taarifa za masuala ya Jiolojia Barani  Afrika hivyo hakikisheni mnaweka mikakati ya kufanya taasisi hii iwe bora zaidi katika sekta ya madini," amesema Mhe. Mavunde.

"Dunia kwa sasa inahitaji Madini ya Kimkakati ikiwemo Kinywe, Lithium na Nikeli kwa ajili ya mahitaji ya Teknolojia ya kisasa na ifikapo mwaka 2050 inategemewa kuwa mahitaji ya madini hayo yatakuwa mara miatatu zaidi ya yalivyo kwasasa," amesema Mavunde.

Aidha, Mhe. Mavunde ameitaka GST kutengeneza mashirikiano na taasisi zingine za utafiti wa Madini duniani kwa lengo la kupata uzoefu, ujuzi na uwezo wa taasisi wa kupata vifaa vya kisasa zaidi na kuwa na Maabara bora Barani Afrika na kuifanya taasisi hiyo kuwa sehemu ya  utambulisho wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya GST Prof. Justinian Ikingula amesema jukumu kubwa la GST ni kufanya utafiti wa jiosayansi kwa lengo la kubaini rasilimali zilizopo ardhini ikiwa ni pamoja na aina za miamba sambamba na madini yanayopatikana kwenye miamba hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchini.

Prof. Ikungula ameongeza kuwa, taarifa za jiosayansi zinazokusanywa na GST ndizo kichocheo kikubwa cha uwekezaji na ukuaji wa Sekta ya Madini nchini ambapo utekelezaji wa majukumu hayo yameifanya GST kuwa kitovu cha taarifa za msingi za jiosayansi ambazo kwa nyakati tofauti zilipelekea gunduzi za migodi mbalimbali ya madini hapa nchini.

Naye, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amewasilisha mada ya mwenendo mzima wa shughuli za Utafiti ambapo amesema lengo la tafiti zinazofanywa na GST ni kuibua maeneo mapya yenye madini na hatimaye kuanzishwa kwa migodi mipya ya uchimbaji wa madini.

Tafiti za jiosayansi ambazo zimefanywa na GST ndizo chanzo cha kuanzishwa kwa migodi mbalimbali nchini kwa kutumia taarifa zake ikiwemo Geita Gold Mine (GGM), Bulyanhulu Gold Mine, Twiga Gold Mine, Nyanzaga Gold Mine, Shanta Gold Mine - Singida, Migodi ya Makaa ya Mawe na sehemu nyingine zenye uchimbaji mdogo na wa kati.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi