Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Finland Yaonesha Nia Kuwekeza Sekta ya Nishati Nchini
Jan 17, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_27238" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akimsikiliza Balozi wa Finland nchini Tanzania, Pekka Hukka (kulia) aliyeongoza Ujumbe wa wawekezaji kutoka Kampuni ya Fortum wakati wa kikao baina yao Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Januari 16 mwaka huu. Kampuni hiyo imeonesha nia kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini.[/caption]

Na Veronica Simba – Dodoma

Ujumbe kutoka Kampuni ya Fortum ya Finland umemtembelea Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na kueleza nia yao kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini.

Ujumbe huo ukiongozwa na Balozi wa Finland nchini Tanzania, Pekka Hukka, ulimtembelea Waziri ofisini kwake mjini Dodoma, Januari 16 mwaka huu.

Akiwatambulisha maafisa aliombatana nao, Balozi Hukka alisema ni wawakilishi kutoka Kampuni ya Fortum inayotoa huduma za nishati ya umeme nchini Finland, ambayo hisa zake nyingi zinamilikiwa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi yenye hisa chache.

[caption id="attachment_27239" align="aligncenter" width="750"] Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka, Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga na Meneja wa Uendelezaji Biashara kutoka Kampuni ya FORTUM ya Finland, Steve Hawes wakijadiliana jambo mara baada ya kikao baina ya Kampuni hiyo na Waziri wa Nishati, kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma hivi karibuni.[/caption]

“Tunatambua umuhimu wa sekta ya nishati katika kuleta maendeleo hususan katika kuwezesha uchumi wa viwanda, ndiyo maana tungependa kuwekeza katika sekta hii,” alisema Balozi Hukka.

Kwa upande wake, Waziri Kalemani aliueleza Ujumbe huo kuwa Serikali ingali inahitaji wawekezaji makini katika sekta ya nishati hususan katika uzalishaji na usambazaji wa umeme.

“Kiasi cha umeme tulichonacho kwa sasa kinaweza kuonekana kutosheleza mahitaji yetu lakini tunajipanga kuzalisha umeme zaidi kwani mahitaji yanazidi kuongezeka siku hadi siku.”

Waziri aliongeza kufafanua kuwa, umeme mwingi zaidi unahitajika hususan kipindi hiki ambapo Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha nchi inaingia kwenye uchumi wa viwanda.

Aliwataka wawekezaji hao kukutana na wataalam kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kujadiliana na kuainisha maeneo mahsusi yanayohitaji uwekezaji.

[caption id="attachment_27240" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akimsikiliza Balozi wa Finland nchini Tanzania, Pekka Hukka na Ujumbe wa wawekezaji kutoka Kampuni ya Fortum (kushoto) wakati wa kikao baina yao Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Januari 16 mwaka huu. Kampuni hiyo imeonesha nia kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini. Kulia ni baadhi ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.[/caption]

Hata hivyo, Waziri aliainisha baadhi ya maeneo muhimu ya sekta ya nishati ambayo yanahitaji uwekezaji kwa sasa ambayo alisema ni pamoja na njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400 kutoka SomangaFungu hadi Dar es Salaam.

Nyingine ni uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe. “Tunayo hazina ya kutosha ya makaa ya mawe huko Magharibi mwa nchi yetu. Hii pia ni fursa nyingine nzuri ya uwekezaji,” alisisitiza.

Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeendelea kuweka mikakati madhubuti inayolenga kuongeza uzalishaji wa umeme na usambazaji katika maeneo yote nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi