Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande amesema Mabadiliko ya tabianchi ni halisi na athari zake tayari zinaonekana sio tu katika mazingira bali pia katika ukuaji wa uchumi na jamii kwa ujumla.
Naibu Waziri Chande amesema hayo wakati wa kufunga warsha iliyofanyika kwa muda wa siku nne kuanzia 3 - 6 Oktoba, 2022 katika hotel ya Kibo Palace, jijini Arusha. Warsha hiyo ilijadili kuhusu upatikanaji wa fedha katika mifuko mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi duniani na maandalizi ya Mkutano wa ishirini na saba wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (cop27)
Ametoa rai kwa washiriki hao kuweka nguvu ya pamoja katika kutafuta rasilimali fedha zitakazowezesha kuwa na ufanisi na tija katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika pande zote mbili za Muungano.
“Kwa niaba ya Wizara ya Fedha ninaomba kuahidi kuwa Wizara itandelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote ili kuiwezesha nchi yetu kuongeza rasilimali fedha na kuwezesha kunusuru hali za jamii zetu tunazoziongoza”, Chande alisitiza.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Omar Shajak amesema katika siku nne za warsha hiyo mijadala mbalimbali juu ya masuala muhimu ikiwemo kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, utekelezaji wa mchango wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) zilijadiliwa.
Mada nyingine ni Mafanikio na changamoto za Miradi mbalimbali ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Usimamizi wa biashara ya Kaboni, Mifumo ya dhamana za bluu (Blue Bond Machanism) na Msimamo wa nchi kuelekea Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika 6-11, Novemba 2022 huko Sharm El Sheikh nchini Misri
Warsha hiyo ya siku nne imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Benki ya Dunia Tawi la Tanzania na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Benki ya Dunia nchini, Wanadiplomasia, Wadau wa Maendeleo, Wakurugenzi kutoka Wizara, Idara na Taasisi zake, wawakilishi wa Benki na Taasisi za Fedha, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia na Wajumbe kutoka Sekta Binafsi.