Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limeahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina mipango ya kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula ndani ya nchi na ziada kuuza nje ifikapo 2030.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Oktoba 16, 2023) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023. Waziri Mkuu amehutubia mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kabla ya ufunguzi wa mkutano huo uliowahusisha Wakuu wa nchi na Serikali, Waziri Mkuu alishiriki katika Maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).
"Pamoja na jitihada ambazo tumeziweka ndani za kushirikisha vijana na wanawake kuhakikisha kwamba tunaongeza teknolojia, kutumia mbolea kwenye kilimo, pamoja na ushirikishaji wa sekta binafsi, tumeamua kuungana na FAO kupitia Mkurugenzi Mkuu na wameahidi kutuunga mkono kwenye Sekta ya kilimo."
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na nishati vijijini ili kurahisisha shughuli za kilimo. “Maboresho mengine ni ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo za kilimo na kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji.”
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt. Qu Dongyu amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa buluu, hivyo Shirika lao liko tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa msaada wa kitaalam pamoja na kukuza mifumo ya uzalishaji wa chakula.
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi alisema kwa sasa Serikali inafanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo na miongoni mwa maboresho hayo ni utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ambayo inalenga kuimarisha upatikanaji wa chakula.
Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema Serikali imeendelea kuwashawishi vijana kushiriki katika shughuli za kilimo kwani mbali na kuongeza uzalishaji wa chakula, pia kilimo ni miongoni mwa sekta zinazotoa ajira nyingi, hivyo watakuwa wamejihakikishia ajira.
Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Italia, Mhe. Sergio Mattarella na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Ireland, Mhe. Michael Higgine, Rais wa Iraq Mhe. Abdul Latif Rashid, Mfalme wa Lesotho, Viongozi wa Ujumbe kutoka Nchi Wanachama, Viongozi Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (FAO, IFAD & WFP).