Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema falsafa za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere bado zina uhalisia kama ilivyokuwa miongo sita iliyopita.
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo Oktoba 14, 2023 mkoani Manyara wakati wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo huambatana na Kumbukizi ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Leo hii inatimia miaka 24 tangu kifo cha Baba wa Taifa, na kila tunapomkumbuka hatuachi kukumbuka misingi ya falsafa zake kama vile Uhuru na Umoja, Uhuru na Kazi, Uhuru na Kujitegemea, Uhuru na Wajibu na mengine mengi aliyokuwa akitueleza”.
“Inawezekana baadhi yetu tukadhani falsafa hizi zimepitwa na wakati na kukosa uhalisia, lakini ukweli ni kwamba kwetu sisi tunaoelewa mienendo na mawanda ya Siasa za Uchumi Kimataifa, falsafa hizi zina uhalisia sasa kama ilivyokuwa miongo sita iliyopita,” amesema Mhe. Dkt. Samia.
Ameendelea kusema kuwa, ili uhuru wetu uwe na maana hatuna budi kudumisha umoja, kuwajibika, kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea. Amesema Serikali inataka kujenga Taifa lenye vijana waadilifu, wawajibikaji, wachapakazi na wazalendo ili waweze kuchangia kikamilifu kwenye maendeleo yao wenyewe na Taifa kwa ujumla.
“Kwa upande wetu Serikali, tumeweka jitihada kubwa katika kuwawezesha vijana wetu kutumia rasilimali nyingi tulizojaaliwa katika Taifa letu ili kujiletea maendeleo na kuboresha maisha yao. Moja ya jitihada hizi ni kutoa elimu ya ujuzi, ambapo tunaendelea na ujenzi wa vyuo vya VETA. ujenzi wa vyuo 64 unaendelea katika wilaya kadhaa na bado tuna deni la vyuo 50. Tunataka kila wilaya iwe na Chuo cha VETA,” amesema Mhe. Rais.
Ameendelea kusema kuwa, wanataka vijana wapate ujuzi utakaowawezesha kuingia kwenye shughuli za ujasiriamali pamoja na uzalishaji wa bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi kama ilivyobainishwa katika Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (Building a Better Tomorrow - BBT) ambayo imeazimiwa kutekelezwa nchi nzima, ambapo tayari utekelezaji umeanza katika baadhi ya mikoa.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema, suala la mazingira ambalo lilikuwa ujumbe mkuu wa mbio za mwenge mwaka huu, bado ni changamoto kubwa katika Taifa.
“Napenda nitumie jukwaa lako kutoa rai kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na kama utaridhia, ujumbe huu uendelee kwa miaka mingine miwili, itusaidie katika kuhakikisha kwamba mazingira ya nchi yetu yanakuwa bora zaidi,” amesema Mhe. Dkt. Mpango.