Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Falsafa za Kimaendeleo za Hayati Mwalimu Nyerere Zinaishi
Oct 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Ni miaka 23 tangu Muasisi na Baba wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atutoka mpaka sasa bado maono na falsafa zake za kuhakikisha nchi ya Tanzana inafika mbali kimaendeleo zinaendelea kuishi kwani viongozi wakuu wanaoendelea kumuenzi kwa vitendo.

Tangu Taifa hili limepata Uhuru, Hayati Mwalimu Nyerere aliwasisitiza wananchi wake kuwa wamoja na kuanza kujitegemea katika kufanya shughuli mbalimbali zitakazoliletea Taifa maendeleo huku akitaka maendeleo hayo kufanyika katika hali ya Uhuru.

Akinukuliwa katika moja ya hotuba zake, Hayati Mwl. Nyerere alisema,”Maendeleo lazima yahusu watu na walete maendeleo yao katika hali ya Uhuru na si kiutumwa na ili tuweze kuendelea kwa Uhuru, ni lazima tutumie kwa hali ya juu kilicho chetu, tutumie mali zetu za nyumbani zikiwemo rasilimali zetu za madini, gesi, ardhi pamoja na wataalam tuliowafundisha wenyewe kabla ya kwenda kutafuta wataalam wengine kutoka nje.”

Katika hotuba hiyo, Hayati Mwl. Nyerere aliendelea kufafanua kuwa maendeleo hayana budi yawe yana uhusiano na maisha ya watu na hakuna budi kuyapima yamefanya nini kwa watu pia kufahamu fedha zimetumiwaje katika kuleta maendeleo kwa watu na kusisitiza kuwa, kama maendeleo hayatokuwa na uhusiano na watu basi sio maendeleo ya kweli.

Falsafa na maono yake katika kipindi cha uongozi wake, vimeendelea kuchagiza maendeleo ya nchi ya Tanzania hata leo ambapo Mwl. Nyerere alisisitiza kuhusu kilimo na tunaona leo Serikali imejikita katika kilimo kwa kuendelea kutenga bajeti kubwa ya kilimo na kusisitiza kulima kilimo cha mashamba makubwa, pia alisisitiza uanzishwaji wa viwanda ambapo Tanzania ya leo imejitahidi kufufua viwanda vilivyokuwepo na kuanzisha vingine vipya.

Alikuwa na maono ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi na leo tunashuhudia Dodoma imekuwa Makao Makuu na shughuli zote za Serikali zikifanyikia hapa.

“Matumaini yangu ni kwamba, kesho na kesho kutwa watu watasema, nendeni muone Watanzania wanavyojenga nchi yao,” alisema Hayati Mwl. Nyerere.

Ni ukweli usiopingika kwamba leo hii Hayati Mwl. Nyerere anapotimiza miaka 23 tangu kifo chake, tunashuhudia na kujivunia maendeleo mbalimbali ambayo mengi msingi wake ulianzia wakati wa uongozi wake ambapo kwa kiasi kikubwa alishughulikia kwa dhati matatizo ya wananchi hasa katika hali zao za kiuchumi na kijamii.

Hata katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020/2025, imesisitiza kutambua umuhimu wa kujenga uchumi wa kitaifa ili kuhakikisha kwamba Watanzania ndio wanufaika wakuu wa uchumi na maliasili za nchi na ndiyo wenye kauli juu ya namna uchumi unavyoendeshwa na kuelekeza Serikali kuendelea na juhudi za kuifanya Tanzania kuwa nchi inayojitegemea kiuchumi pamoja na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na nchi nyingine ambapo juhudi maalum zitaelekezwa kuhakikisha rasilimali za asili za nchi hii, hasa ardhi, madini, gesi asilia, mafuta, maji na misitu zinanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.

Miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa nchini ikiwemo ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, ujenzi wa shule na vyuo, miradi ya maji na umeme, miundombinu ya barabara na madaraja lakini Tanzania inatekeleza pia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Makao Makuu ya nchi, mradi wa Umeme wa Mto Rufiji, ujenzi wa reli ya kisasa – SGR, Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege, upanuzi wa bandari, ukarabati na ujenzi wa meli mpya na ununuzi wa ndege mpya na rada.

Yote haya ni kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo. Mwalimu tutakukumbuka daima.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi