Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema falsafa yake katika kutekeleza majukumu yake ni bidii katika kazi, kufanya kazi kwa umoja pamoja na ustawi wa watumishi.
Waziri Dkt. Ndumbaro amesema hayo Septemba 04, 2023 wakati wa makabidhiano ya ofisi ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye amehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria.
“Falsafa yangu katika kazi ina mambo matatu, ‘hard work’, kwenye kazi mimi ni mtu wa kazi kazi, ‘team work’, kufanya peke yako haina maana, kufanya kazi kwa pamoja tutafika mbali na kwa ufanisi, na ‘welfare’, sote tuna kila sababu ya kufurahia matunda ya kazi yetu”, amesema Dkt. Ndumbaro.
Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa hajawahi kupokelewa kwa bashasha tangu ameanza kufanyakazi baada ya kuteuliwa kutumikia wizara mbalimbali na kuongeza kuwa amepata pongezi kutoka taasisi mbalimbali na wadau hatua inayoonesha watu wana matumaini kwa kuteuliwa kwake kuiongoza wizara ambapo amewasihi menejimenti na watumishi wa wizara hiyo kutekeleza majukumu yao ili kuwahudumia watanzania.
Akikabidhi ofisi, Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye amehamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria amesema kuwa Wizara hiyo inawawakilishi kila wilaya na mikoa yote nchi nzima maafisa Utamaduni na Michezo ambao wanawahudumia watanzania katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema kuwa hiyo ni Wizara ya furaha ambapo amesisitiza kuwa wakati watu wanaburudika, viongozi na watumishi wa wizara hiyo wanakuwa kazini kutekeleza majukumu yao pamoja wadau.
Awali akimkaribisha Mhe. Waziri, Dkt. Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu ametoa kwa ufupi wasifu wa Dkt. Ndumbaro na kusisitiza kuwa Waziri huyo ni mtendaji mzuri na mdau mkubwa wa michezo wa miaka mingi na ni mwanamichezo mzuri wa mchezo wa gofu ambapo amemuahidi kuwa atapata ushirikiano kwani menejimenti na watumishi wa wizara hiyo wapo tayari kupokea maelekezo atakayotoa na kuyatekeleza.