Bi. Rahabu Daudi, Mhasibu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Busega moja kati ya washiriki wa mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma akitoa msaada kwa washiriki wenzake.
Na: Gladys Mkuchu - PS3
TAMISEMI kwa kushirikia na Serikali ya Marekani kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), umewezesha Halmashauri zote nchini kushiriki mafunzo ya uelewa juu ya mabadiliko na maboresho yaliyofanyika katika mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma (EPICOR Toleo 10.2).
Maboresho ya mfumo huu wa fedha yanatokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili watendaji wanaotumia mifumo hiyo.
“Mfumo wa EPICOR 10.2 utaturahisishia sana utendaji wa kazi, mfano mzuri ni kwenye upande wa mapato ambapo hapo awali ilikuwa ngumu kuhamisha taarifa kutoka mifumo mingine ya kifedha na kuingiza kwenye mfumo wa awali. Lakini kupitia huu ulioboreshwa ambapo unaingiza taarifa moja kwa moja kutoka mifumo mingine utarahisisha sana kazi,” amesema Rahabu Daudi, Mhasibu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
Mhasibu kutoka TAMISEMI, Melkzedeck Kimaro ambaye ni mwezeshaji kwenye mafunzo ya mfumo wa EPICOR 10.2 Mkoani mwanza akitoa msaada wa kiufundi kwa washiriki.
Ameeleza kuwa, kutokana na kurahisishwa kwa utendaji wa kazi tutaweza kupata muda kuweza kutekeleza majukumu mengine hususani katika kutoa huduma kwa wananchi ambapo hapo awali wakati wa kufanyia kazi mfumo huu ililazimu kuahirisha huduma kwenye halmashauri zetu kutokana na kuwa na majukumu mengi katika kuingiza taarifa katika mfumo.
“EPICOR 10.2 hii iliyoboreshwa imehuishwa na mifumo mingine ya fedha katika halmashauri kama vile Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato (LGRCIS), Mfumo wa Usimamizi/Uendeshaji wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya, ambao unapokea mapato ya papo kwa papo (cost sharing) na kutunza taaarifa za wagonjwa (GoT-HoMIS), mfumo wa taarifa za kihasibu kwenye Vituo vya Kutolea Huduma (FFARS) pamoja na mfumo ulioboreshwa wa kuandaa Mipango na Bajeti (PlanRep). Kuwepo na mfumo unaowasiliana na mifumo mingine utawarahisishia sana watendaji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa muda mfupi sana,” amesema Bw. Aloyce Maziku, Mshauri wa mambo ya Fedha PS3. Baadhi ya washiriki mkoani mwanza wakiendelea na mafunzo ya vitendo ya Mfumo wa EPICOR 10.2. Mmoja wa washiriki akifuatilia mafunzo kwa vitendo ya Mfumo wa EPICOR 10.2 yanayoendelea mkoani Mwanza.Naye Bw.Stanslaus Msenga, Mhasibu Daraja 1 kutoka TAMISEMI ambaye ni Mkufunzi wa Mafunzo haya amesema, Mfumo haujawarahisishia tu watendaji katika Halmashauri lakini pia na Serikali kuu yaani TAMISEMI ambapo utawezesha kufuatilia kwa urahisi Hesabu za Halmashauri, pia utatoa taarifa za utekelezaji za mipango na bajeti kwa kuzingatia matumizi ya fedha yaliyofanyika na pia kurahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika ngazi ya Serikali za Mitaa mpaka ngazi ya vituo vya kutolea huduma.
Ameongeza kuwa, mfumo huu utasaidia pia hata wakaguzi kuweza kufanya ufuatiliaji wa moja kwa moja sababu mfumo huu unajumuisha masuala yote ya fedha katika halmashauri zetu nchi nzima hivyo kumbukumbu na taarifa zote zinaweza kupatikana kwa urahisi sana na hivyo kurahisisha zoezi la ukaguzi wa fedha nah ii itachochea pia Halmashauri kuondoa hati chafu.