[caption id="attachment_27245" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Solutions Tanzania Ltd, Neithan Swedy akionesha kwa waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam njia ya kutuma maombi ya masomo katika vyuo vya nje ya nchi kupitia tovuti ya taasisi hiyo (www.elimusolutions.co.tz) pamoja na taratibu mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa na waombaji.[/caption]
Na Ismail Ngayonga.
TAASISI ya Elimu Solutions Tanzania Ltd imewataka Wafanyakazi na Wajasiriamali wa Tanzania kuchangamkia fursa za ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi katika kada mbalimbali yanayotolewa na Vyuo Vikuu mbalimbali katika Jamhuri ya Watu wa China ili kujiongezea ujuzi na maarifa katika utendaji kazi wao.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Bw. Neithan Swedy wakati wa mkutano wake na waandishi wa vyombo vya Habari na kuongeza kuwa dirisha la maombi hayo linatarajia kufunguliwa mwezi Juni mwaka huu.
Swedy alisema taasisi yake tayari imefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa fursa hiyo, ambapo imefanya mawasiliano na Vyuo vikuu na makampuni mbalimbali kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali ikiwemo maradhi na usafiri wakati wa mafunzo hayo.
[caption id="attachment_27246" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Solutions Tanzania Ltd, Neithan Swedy akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kwa zoezi la kutuma maombi ya udahili wa masomo kwa wanafunzi wa nje ya nchi (China, Japan na Korea Kusini) pamoja na taratibu mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa na waombaji. Kulia Afisa Tawala wa Taasisi hiyo, Irene Kigwangwa.[/caption]“Mwaka jana tulipokea maombi mengi ya Wafanyakazi na Wajasiriamali wakiiomba taasisi yetu kuwawezesha kupata mafunzo ya muda mfupi, ambapo nasi tumesikia maombi yao na tutatangaza tarehe maalum ya kuanza kupokea maombi hayo” alisema Swedy.
Aidha aliwataka wanafunzi na waombaji wa nafasi za masomo katika Taasisi za Elimu nje ya nchi ikiwemo Vyuo Vikuu kuwa makini na baadhi ya kampuni za uwakala kwa kuwa zipo baadhi ya kampuni zimekuwa zikiwatapeli waombaji.
Kwa mujibu wa Swedy ili kujiridhisha na uhalali wa Kampuni za Uwakala wa vyuo vya nje ya nchi, waombaji wanapaswa kuhoji baadhi ya nyaraka muhimu kutoka kwa kampuni hizo ikiwemo leseni ya biashara, Namba ya Utambulisho ya mlipa kodi na muhuri maalum kutoka Wizara ya Mamboya Ndani na pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Alisema Taasisi yake haichukui ada yoyote ya mwanafunzi badala yake inatoza ada ya uwezeshaji pamoja na gharama za usafiri katika kipindi ambacho mwanafunzi anapofika katika nchi husika na ada ya masomo yake huilipa mwanafunzi katika Chuo alichopatiwa udahili.
[caption id="attachment_27247" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Solutions Ltd, Neithan Swedy akionyesha kwa waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam nyaraka ya Namba ya Utambulisho Mlipa Kodi (TIN) inayotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) na kupaswa kuwa nayo kila kampuni ya uwakala wa utafutaji wa nafasi za masomo katika vyuo vya nchi za nje ya Tanzania. Wengine ni Afisa Tawala Irene Kigwanga na Meneja mwendeshaji wa Elimu Solutions, Ibrahim Swedy.[/caption]Kuhusu udahili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza, Swedy aliwataka waombaji kuanza kutuma maombi ya masomo katika nchi za China, Japan na Korea kupitia tovuti ya taasisi hiyo (www.elimusolutions.co.tz) kuanza sasa hadi Mwezi machi mwaka huu na baadae waombaji wa shahada ya uzamili kuanzia mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu.
Anasema hadi sasa Taasisi hiyo imeweza kusafirisha jumla ya wanafunzi 132 katika nchi ya China, na kusema taasisi hiyo ina uwezo wa kuwasaidia wanafunzi 1500 kupata nafasi za ufadhili wa masomo katika nchi hizo za Bara la Asia.
Swedy aliongeza kuwa kutokana na kuongeza kwa soko la mahitaji ya ufadhili wa masomo nje ya nchi, taasisi hiyo inaendelea kufanya mazungumzo na Vyuo mbalimbali vilivyopo katika nchi za Uingereza na Marekani, mchakato ambao upo katika hatua nzuri za mafanikio.
Aliwataka wazazi na walezi nchini kuondoa uwoga kwa kusomesha watoto wao nje ya nchi kwani kwa sasa ada ya masomo katika nchi hizo inafanana na ada zilizopo katika vyuo vikuu vya Tanzania na kuwataka wanafunzi kuchangamkia fursa hiyo.