Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DP World Kuongeza Mapato kutoka Trilioni 7.7 hadi Trilioni 26.7 Ifikapo 2032
Jul 14, 2023
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam

Serikali imewataka wananchi kutokuwa na hofu kuhusu uwekezaji utakaoingiwa na Serikali ya Tanzania na Kampuni ya uendeshaji wa bandari ya DP World kwani uwekezaji huo utakuwa na manufaa makubwa katika ukusanyaji mapato ya Serikali.

Akizungumza katika Mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa uwekezaji huo utakuwa na manufaa kwa taifa katika kupata fedha kwa kukusanya kodi kupitia ushuru wa forodha.

“Uwekezaji huu utakaofanywa na kampuni ya DP World katika bandari yetu ya Dar es Salaam utaongeza shehena zitakazokuwa zikihudumiwa katika bandari yetu kutoka tani milioni 18.4 za mwaka 2021 hadi tani milioni 47.5 mwaka 2032 sawa na asilimia 198, hii itaongeza mapato kupitia ushuru wa forodha kutoka trilioni 7.76 mwaka 2021 hadi trilioni 26.7 mwaka 2032 sawa na asilimia 244”, Alisema Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa alisema kuwa, uwekezaji huo utapunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 mpaka saa 24 jambo ambalo litapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za utumiaji bandari hiyo, lakini pia uwekezaji huo utaogeza meli zinazokuja katika bandari hiyo kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 hadi meli 29,570 ifikapo mwaka 2032.

Aidha, Waziri Mbarawa alisema uwekezaji wa DP World katika Bandari ya Dar es Salaam, utaongeza ajira ambazo zitawafanya Watanzania kupata kipato wao binafsi kutoka katika shughuli za kila siku za bandari

“Uwekezaji huo wa DP World utaongeza ajira zitokanazo na shughuli za bandari kutoka ajira 28,990 za mwaka 2021 hadi kufikia ajira 71,907 ifikapo mwaka 2032 sawa na ongezeko la asilimia 148”, Prof. Mbarawa.

Mbarawa aliongeza kuwa, DP World itapunguza ushushaji wa makasha kutoka siku 4 hadi 5 mpaka siku mbili  na pia kupunguza muda wa kuondoa mzigo bandarini kutoka saa 12 hadi saa 1 kutokana na kuimarishwa kwa mifumo ya TEHAMA katika bandari hiyo.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi