Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma
Mkoa wa Dodoma umefanikiwa kujenga viwanda 892 vingi kati ya hivyo vikiwa ni Vidogo na vya Kati ambavyo vinachochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kutekeleza dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Akizungumza katika Kipindi maalum cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge amesema kuwa Mkoa huo umejipanga vyema kama Makao Makuu ya Nchi kuhakikisha kuwa dhana ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda inatekelezwa na wananchi wote kwa vitendo .
Akifafanua zaidi Dkt. Mahenge amesema kuwa Dodoma ni mahali salama na kuna maeneo yakutosha kwa ajili ya uwekezaji hivyo wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi wanakaribishwa kuja kuwekeza.
“Dodoma tayari tumeanza kutekeleza miradi inayochochea maendeleo ya uchumi wa viwanda na tunaamini kuwa Dodoma itakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kiunganishi cha mikoa yote nchini” Alisisitiza Dkt. Mahenge
Aliongeza kuwa ni vyema Vijana wanaoishi Mkoani Dodoma wakajiunga katika kwenye Vikundi ili wapatiwe ujuzi utakaowawezesha kujikwamua kiuchumi ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo na shughuli za uzalishaji kwa ujumla.
Pia aliwaasa wanaotaka kujenga Mkoani Dodoma kuzingatia Mpango Mji (Master Plan) kwa kuwa Serikali imeshapanga na itasimiamia mpango mji uliopo kwa faida ya wananchi wote.
Akitolea mfano suala la kumiliki Ardhi Mkoani Dodoma Dkt. Mahenge alisema kuwa ni muhimu kupitia Manispaa ili kuepuka utapeli na usumbufu unaoweza kujitokeza baadae ikiwa taratibu hazitafuatwa katika kumiliki Ardhi.
Katika kuhakikisha kuwa Makao Makuu ya nchi yanakuwa katika mpangilio unaovutia tayari Serikali imepima viwanja kwa ajili ya kujenga majengo ya Ofisi za Wizara , Taasisi na Balozi zote katika eneo maalum utakapojengwa mji wa Serikali.
Kipindi cha TUNATEKELEZA kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawashirikisha wakuu wa Mikoa yote, baada ya awamu iliyotangulia kuwahusisha Mawaziri wote na watendaji wengine wa Serikali.