*Asema Mkesha Mkubwa wa Kitaifa mwaka huu utafanyika Dodoma
ASKOFU wa Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches (TFC), Dk. Godfrey Mallasy amesema Jiji la Dodoma kwa sasa ni shwari na liko tayari kwa ujio wa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
Ametoa kauli hiyo jana jioni wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye kanisa la Dodoma Christian Centre mara baada ya kumaliza ibada maalumu ya kuombea ujio wa Rais Magufuli jijini Dodoma.
Askofu Mallasy alikuwa akihitimisha semina ya siku nne ya jinsi ya kutambua madhabahu zinazokutesa na kuzivunja na kisha kufunguliwa.
Alisema TFC iliandaa semina hiyo kwa kushirikiana na makanisa mengine na kuamua kuhitimisha kwa maombi ya kuvunja madhabahu za mkoa wa Dodoma na kujenga madhababu ya kitaifa.
“Ndoto ya Serikali kuhamia Dodoma inakaribia kutimia kwa sababu wizara zote zimeshahamia hapa na Mheshimiwa Rais wetu anakaribia kuhamia. Kwa hiyo, viongozi wa kiroho tunao wajibu wa kumuandalia makazi yake ya kiroho. Jambo lolote likitokea, basi ujue limeanzia rohoni,” alisema.
“Leo tuko Dodoma, madhabahu ya hapa inasema kila kitu kitadidimia (kutokana na asili ya neno Dodoma – idodomya- linalomaanisha kudidimia). Na falme za hapa zimetamka hilo lakini baada ya maombi haya, sisi tunasema Dodoma haitadidimia, bali itaamka.”
Alisema maneno hayo kupinga hali ya uduni wa Dodoma, yanaendana na ujasiri wa Serikali ya awamu ya tano kuhamishia shughuli zake zifanyike makao makuu ya nchi, Dodoma.
“Rais wetu anakuja hapa na ana ndoto kubwa, je ndoto hizo zitaenda wapi? Jeshi la Mungu liko hapa, kwa hiyo ndoto hizo hazitadidimia kama jina lilivyo. Kupitia kuangusha ngome na madhababu za Dodoma, mambo yanaenda kubadilika,” alisisitiza.
Alisema maombi hayo yamefanyika ili Rais Magufuli aweze kutawala kwa amani na kutekeleza ndoto zake za kuijenga Tanzania mpya kwa mafanikio makubwa. Alisisitiza Watanzania wote, kuanzia kwenye ngazi ya familia, waendelee kuliombea Taifa liwe na amani kwa sababu pasipokuwa na amani, hakuna kinachoweza kufanyika.
Mapema, katika ibada hiyo, Askofu Mallasy aliwaongoza wachungaji wengine 20 wa TFC kutoka mikoa mbalimbali nchini pamoja na wachungaji kutoka makanisa ya FPCT, EAGT, TAG, KKKT na Anglikana kuimba wimbo wa Taifa na kufanya kitendo cha kumpokea Rais Magufuli.
Pia aliongoza waumini mbalimbali waliohudhuria ibada hiyo kuvunja madhabahu kwenye mihimili yote mitatu ya nchi yaani mahakama, Bunge na Serikali kwa kutaja wizara mbalimbali, kuwaombea wakuu wa mikoa yote, wilaya zote, wakurugenzi wa halmashauri zote za Majiji, miji, manispaa na wilaya.
Wakati huohuo, Askofu Mallasy ametangaza kwamba Mkesha Mkubwa wa Kitaifa ambao hufanyika tarehe 31 Desemba kila mwaka kwa ajili ya kuliombea Taifa, mwaka huu utafanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mkesha wa kuliombea Taifa, umekuwa ukifanyika nchini kila mwaka kuanzia mwaka 1997.