Viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekusanyika jijini Dodoma leo katika hafla maalum ya kumpokea Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson akitokea nchini Angola ambapo uchaguzi wa Urais wa Umoja huo umefanyika.
Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amemuomba Dkt. Tulia kuhakikisha anaipigania Tanzania katika mikutano yote ya Umoja wa Taifa ambapo atakuwa akiingia kupitia cheo chake.
“Moja ya majukumu yako yaliyozungumzwa hapa ni kwamba utakuwa ukihudhuria vikao vyote vya Umoja wa Mataifa, na sote tunajua kwamba tumesaini mikataba mingi katika umoja huo kwenye nyanja mbalimbali, tunashukuru kwa kuwa tutakutumia wewe Rais wa Mabunge Duniani ili upeleke ajenda za Taifa kwenye vikao vya Umoja wa Mataifa,” ameeleza Waziri Mkuu.
Akitoa neno la shukrani, Mhe. Dkt. Tulia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia awe mgombea wa nafasi hiyo.
Naye, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Iddi Azan Zungu amewaomba wabunge na wananchi wote kuendelea kushirikiana na Dkt. Tulia katika kulijenga Taifa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mhe. Oran Njeza amesema ushindi wa Dkt. Tulia umetokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha diplomasia.