Na: Tiganya Vincent
Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania imetakiwa kufuatilia utendaji wa watendaji na watumishi wa chombo hicho kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanafanyakazi kwa uadilifu na kuzingatia uzalendo.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Tabora na Waziri wa Kilimo Dkt.Charles Tizeba wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku ya Tanzania.
Alisema kuwa kama wapo watumishi ambao sio waadilifu wala sio waaminifu wachukuliwe hatua mapema kabla ya mambo hayajaharibika zaidi.
Dkt. Tizeba aliongeza kuwa sio vizuri kugonja viongozi wakuu kuja kuchukua hatua wakati wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ipo.
“Msingoje Waziri au Waziri Mkuu au Rais ndio aje kuchukua hatua …ukiona hilo linatokea mjue nyinyi kana Wajumbe wa Bodi hamjafanyakazi yenu …Rais anakuja kwenye mkutano
Alisema kuwa ukiona wananchi wanaonyesha mabango ujue kuwa viongozi wa pale shughuli imewashinda ndio maana wanangoja Rais au Waziri Mkuu aende ndio yaandikwe.
Dkt. Tizeba aliwaambia wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wajitahidi kushughulikia matatizo mapema na sio kusibiri viongozi waende na wananchi waonyesha mabango ndio waanze kuchukua hatua.
Naye Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Hassan Wakasubi alisema kuwa hatasita kuwachukulia hatua watumishi wa Bodi hiyo ambao watakuwa hawafanyi kazi kwa weledi na wale wanaoonekana kutoendana na kasi ya Awamu ya Tano.
Aliongeza kuwa katika kipindi chao cha uongozi watasaidia utatuzi wa matatizo mbalimbali yanayoikabili Bodi hiyo ikiwemo ukosefu wa Jengo kubwa kwa ajili ya kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Wakasuvi alisema kuwa lengo ni kutaka kurudi hadhi ya kilimo cha tumbaku ili kiwezo kuwa ndio namba moja katika kuingiza fedha za kigeni hapa nchini kama ilivyokuwa miaka ya hivi karibuni.
Alisema kuwa ili kufanisha hilo itawalazimu kuvitembelea vyama vya msingi vyote hapa nchini vinavyojishughulisha na kilimo cha tumbaku kwa lengo la kujadiliana juu ya uboreshaji wa zao hilo ili liweze kumsaidia mkulima kuondokana na umaskini.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggery Mwanri alisema kuwa baada ya uteuzi wa Bodi ya Wakurugenzi itasaidia kumpunguzia kazi ya kukabiliana na matatizo mbalimbali ya wakulima wa tumbaku yaliyokuwa yakipelekwa kwake.
Alisema kuwa wakulima sasa watakuwa na watetesi pindi wanaponyanyasa na viongozi wa vyama vyao vya msingi .