Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Possi Awataka Wananchi Kulinda Miundombinu ya Reli.
Oct 15, 2023
Dkt. Possi Awataka Wananchi Kulinda Miundombinu ya Reli.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Ally Possi, akiongea na Uongozi pamoja na Kukagua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na kusimamiwa na Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL), ikiwemo ukarabati wa Meli ya Mafuta ya MT SANGARA ambayo ukarabati wake umefikia asilimia 92 mkoani Kigoma.
Na Mwandishi Wetu

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Ally Possi amewataka wananchi kuhakikisha wanakuwa walinzi wa miundombinu ya reli kwa ajili ya maendeleo ya nchi na kuhakikisha usalama wa watumiaji.

Dkt. Possi ametoa wito huo leo alipozungumza na wananchi wa Mkoa wa Tabora pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli yalioanza Oktoba 9, 2023 na kufanyika kitaifa mkoani humo.

"Miundombinu hii ni gharama kubwa sana, hivyo nitoe rai kwa wafanyakazi na sisi sote kwa ujumla kutunza miundombinu hii kwani tunapoiharibu ndipo pia tunapohatarisha usalama wa usafiri wa reli," Amesisitiza Dkt. Possi.

Aidha, Possi amesema kuwa endapo mtu atahujumu miundombinu ya reli huo ni uhalifu na uhujumu uchumi na kusisitiza kuwa kama serikali haiwezi kuvumilia uhalifu huo huku akisisitiza kuwa maeneo yote ambayo gharama ya usalama wa reli zimeondolewa ni vema zikarejeshwa mara moja ili kuimarisha usalama wa reli.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRC), Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Reli Tabora, Damas Mwajanga amesema TRC linaendelea na jitihada mbalimbali za kuimarisha shirika hilo ikiwemo ukarabati wa miundombinu ikiwa ni pamoja na mabehewa na vichwa vya treni.

"Tunapenda kuwakumbusha wananchi kuwa katika usafiri wa reli usalama ni kipaumbele cha kwanza, hivyo wazingatie matumizi sahihi ya ishara na alama katika maeneo ya vivuko, hifadhi ya reli, stesheni na maeneo ya hifadhi ya reli," Amesema Mwajanga.

Maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli ni matokeo ya Maazimio ya Shirikisho la Mashirika ya Reli Kusini mwa Afrika (SARA) ambalo Tanzania ni mwanachama ambapo huadhimisha wiki hiyo mwezi Oktoba ya kila mwaka, katika mwaka huu maadhimisho hayo yameongozwa na kauli mbiu isemayo " Usalama wa reli unaanza na wewe, chukua tahadhari".

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi