Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Ndumbaro Ateta na Balozi Mehmet wa Uturuki
Oct 03, 2023
Dkt. Ndumbaro Ateta na Balozi Mehmet wa Uturuki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akisalimiana na Balozi wa Uturuki hapa nchini, Mhe. Dkt. Mehmet Gulluoglu baada ya kumaliza majadiliano yao leo Oktoba 3, 2023 Jijini Dar es Salaam. Mwenye suti kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa.
Na Shamimu Nyaki

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Oktoba 3, 2023 Jijini Dar es Salaam amefanya mazungumzo na Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Dkt. Mehmet Gulluoglu, ambapo wamekubaliana kushirikiana katika eneo la Utamaduni na Michezo.

Mhe. Dkt. Ndumbaro amemueleza Balozi huyo kuwa Tanzania inaendelea kupiga hatua katika eneo la Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo Sekta hizo sasa ni biashara na zinatoa ajira kwa vijana wengi, huku akisema lugha ya Kiswahili inaendelea kukua na kuongeza idadi ya wazungumzaji.

Kwa upande wake Balozi Mhe. Mehmet amesema nchi yake itaisaidia Tanzania kuanzisha Kituo cha Utamaduni hapa nchini, ambapo amesema kituo hicho kitatoa fursa kwa waturuki kujifunza kiswahili na Watanzania kujifunza Kituruki.

Ameongeza kuwa, nchi hiyo ipo tayari kusaidia ujenzi wa vituo vya michezo na kwamba  klabu ya Fernabache ya nchini humo ina nia ya kuanzisha akademi ya michezo hapa nchini.

Aidha, Mhe. Mehmet amesema kupitia ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo, timu za Tanzania zitaendelea kupewa kipaumbele kuweka  kambi za maandalizi ya michezo mbalimbali  nchini humo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi