Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Ndugulile: Endeleeni Kutibu Watu Wenye Magonjwa Mengine na si wa Covid -19 Tu
May 07, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na John Stephen, WAMJW – Dar es Salaam

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewataka wataalam wa afya kuendelea kutibu watu wenye magonjwa mengine kama vile matatizo ya moyo na figo katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Covid-19.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile baada ya kuitembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuwaona wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo.

Dkt. Ndugulile amesema pamoja na kuwapo kwa maambukizi ya ugonjwa wa Corona, watu wenye matatizo ya moyo, kupumua, figo, kisukari pamoja na matatizo mengine wanapaswa kupatiwa matibabu.

“Tunaweza tukawa tunapambana na Corona, tukawapoteza wagonjwa wengi kwa sababu tu hatujaweza kuwapatia huduma ya matibabu ya kisukari, figo, presha au moyo, hivyo nitoe rai kwa wahudumu wa afya wahakikishe wanaendelea kuwatibu watu wenye magonjwa haya pamoja na magonjwa mengine,” amesema Dkt. Ndugulile.

Katika hatua nyingine, Dkt. Ndugulile amewapongeza wataalam wa JKCI kwa kufanya upasuaji wa kupandikiza mishipa kwenye moyo kwa wagonjwa waliokuwa na matatizo ya moyo.

 “Sisi kama Wizara ya Afya, tunapata faraja sana, mambo kama haya ni mazuri na lazima tuseme kwa hiyo hii operesheni mliofanya ni kubwa na nje ya nchi ingetugharimu shilingi milioni 80 hadi 90 kwa mtu mmoja, lakini hapa tumefanya kwa shilingi milioni 29 kwa kutumia wataalamu wetu na wagonjwa wetu wanaendelea vizuri,” amesema Dkt. Ndugulile.

Amesema awali wataalam kutoka nje ya nchi walikuwa wanakuja kufanya upasuaji kama huo, lakini sasa Watanzania wazalendo wanafanya baada ya kutoa mishipa kwenye paja na kwenye kifua cha mgonjwa husika.

“Leo nimekuja kuona kazi kubwa iliyofanywa na wataalam wazalendo wa JKCI ya upasuaji wa kupandikiza mishipa kwenye moyo ili uweze kufanya kazi kwa wagonjwa waliokuwa wakikabiliwa na matatizo ya moyo,” amesema Dkt. Ndugulile.

Naye Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI, Dkt. Angella Muhozya amesema kuwa wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji na wataalamu wazalendo wanaendelea vizuri na kwamba wataruhusiwa muda wowote kuanzia sasa.

Mmoja wa wagonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa moyo, Bw. Hamid Nassoro amesema baada ya kufanyiwa upasuaji hivi sasa anaweza kuzungumza vizuri tofauti na awali alikuwa hawezi kuzungumza na kwamba tayari ameshaanza mazoezi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi