Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Nchemba Awahimiza Wakuu wa Mikoa Kusimamia Sensa Kikamilifu
Jul 28, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Saidina Msangi, WFM, Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, (Mb), amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia kikamilifu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili kuwezesha kupatikana kwa takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali katika upangaji wa mipango ya maendeleo.

Maagizo hayo aliyatoa wakati akifunga mafunzo ya siku 21 kwa Wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi ngazi ya mkoa Kitaifa katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Alisema kuwa Serikali imedhamiria kujenga uchumi endelevu na kupunguza umaskini kwa wananchi hivyo matokeo ya Sensa hiyo ndio dira ya kupanga mipango ya maendeleo endelevu ya wananchi.

“Mkuu wa Mkoa ambaye Mkoa wake watu hawatashiriki ipasavyo kuhesabiwa ajue kuwa mipango ya maendeleo ya mkoa wake haitaenda sambamba na idadi ya watu waliopo, mfano huduma za shule, maji, afya, umeme hazitatolewa kuendana na uwiano wa watu waliopo na hatutegemei kuona hili jambo likitokea katika utekelezaji wa Sensa hii” alisisitiza Dkt. Nchemba.

Alisisitiza kuwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la Kitaifa na Kimataifa hivyo ni muhimu kulitekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu kwa lengo la kutekeleza matakwa ya Umoja wa Mataifa ambapo Tanzania ni Wanachama.

Aidha, Dkt.Nchemba aliwapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuwa miongoni mwa watu 11,000 kati ya mamilioni ya Watanzania ambao wangeweza kuchaguliwa kushiriki mafunzo hayo na kuwaasa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Nina Imani elimu mliyoipata mtaipeleka ipasavyo katika ngazi ya makarani na wasimamizi kwa lengo la kuwapata makarani ambao watakusanya taarifa za kitakwimu zinazokidhi vigezo vyote vya Kanuni za Umoja wa Mataifa’, Alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alitoa rai kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23 mwaka huu ya kidigitali na inaunganisha mazoezi mawili makubwa ya kitaifa ambayo Sensa ya Majengo yote Nchini, na Sensa ya Anwani za Makazi, ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu zitakazosaidia katika upangaji wa bajeti na mipango yha maendeleo.

Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Mhe. Anna Makinda, aliwaasa Wakufunzi hao wanapoenda kutoa elimu kwa makarani wa sensa kuzingatia sifa za washiriki na kutosita kuchukua hatua kwa washiriki wasio na sifa.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa, alisisitiza umuhimu wa zoezi la Sensa kwamba ni takwa la kisheria na pia ni makubaliano ya Umoja wa Mataifa na inatumika kuipima nchi katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na NBS ambapo lengo  lake lilikuwa ni kujenga uelewa mpana na wa pamoja kwa wahusika kupata kanuni na mbinu bora za namna ya kukusanya taarifa za kitakwimu nchi nzima kwa kufuata Kanuni za Umoja wa Mataifa.

Aidha, Wahitimu hao wanatarajiwa kwenda kufundisha Makarani na Wasimamizi wa Sensa wapatao 205,000 kwa nchi nzima.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi