Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa wito kwa Kampuni ya Mawasiliano ya Huawei ya China, kuisaidia Tanzania kuweka mifumo ya kisasa ya teknolojia ya Mawasiliano itakayowezesha nchi kuboresha ukusanyaji mapato yake ya ndani na kupunguza malalamiko ya watumiaji wa mifumo hiyo wakiwemo wafanyabiashara.
Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo Beijing nchini China alipoongoza Ujumbe wa Tanzania kutembelea Kampuni hiyo Tawi la Beijing ambapo masuala kadhaa ya uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Tanzania, yalijadiliwa.
Alisema kuwa mifumo iliyopo nchini ya kukusanya mapato ya ndani ya Serikali haisomani (haiwasiliani ipasavyo) na kuzuia malalamiko kutoka kwa watumiaji lakini pia hali hiyo inaikosesha Serikali mapato.
Dkt. Nchemba aliyeambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu Elimaamry Mwamba, Balozi wa Tazania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki na Viongozi wengine Wakuu wa Taasisi za Serikali ikiwemo TANROADS na Shirika la Reli Tanzania (TRC), alisema kuwa ujumbe wa Tanzania umejionea mageuzi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA iliyobuniwa na Kampuni hiyo.
Alisema kuwa miaka michache iliyopita Kampuni hiyo ilikuwa ni ya kawaidia lakini baada ya kuwekeza kwenye utafiti wa teknolojia janja, Huawei imekuwa Kampuni kubwa na inayoheshimika ulimwenguni na kwamba inaweza kuisaidia Tanzania kuboresha mifumo yake ya ukusanyaji mapato yake kwa njia ya kodi mbalimbali.
Aidha, Dkt. Nchemba ameuomba uongozi wa Kampuni hiyo ambao uliongozwa na Makamu wake wa Rais, Bw. Zhang kwenye mazungumzo hayo, kutoa nafasi kwa vijana wa kitanzania za kuongeza ujuzi wa masuala ya TEHAMA kwa kuwapa nafasi ya kujifunza kwa vitendo kwenye Kampuni hiyo ili nchi iwe na vijana wabobezi kwenye masuala ya mawasiliano hivo kukuza ajira na kujiongezea kipato.
Aliiomba pia Kampuni hiyo kuwekeza nchini Tanzania kwa kujenga kiwanda cha kutengeneza simu janja ili wananchi hususan waishio vijijini wapate simu janja kwa bei nafuu na ziwasaidie katika kazi zao za kujipatia kipato na kwamba soko kubwa la ndani ya nchi na nchi jirani ni kivutio kikubwa cha uwekezaji huo.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa HUWAEI, Bw, Zhang, Meneja wa Huawei Tawi la Tanzania, Bw. Russel Zhao, alisema kuwa Kampuni yake imepokea maombi ya Serikali kupitia kwa Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na kwamba itaangaza fursa mbalimbali zinazopatikana nchini Tanzania na kuwekeza mitaji na teknolojia.
Alisema kuwa uhusiano mzuri na wa muda mrefu uliopo kati ya China na Tanzania unaendelea kuleta hamasa na kwamba Kampuni hiyo itaangalia uwezekano wa kurejesha Ofisi yake Tanzania kwa hivi sasa wanafanya shughuli zao nchini Tanzania kutokea nchi Jirani ya Kenya.