Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewahakikishia wawekezaji kutoka Uingereza na Norway kwamba Serikali itatoa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha uwekezaji wao hapa nchini kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji pamoja na vivutio kadhaa.
Dkt. Nchemba ametoa ahadi hiyo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na kundi la wawekezaji kutoka nchini Uingereza na Norway, wanaotaka kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa nchini.
Ujio wa wawekezaji hao wanaotaka kuwekeza kwenye sekta za kilimo, nishati, uchimbaji na uchakataji madini, ujenzi wa miundombinu mbalimbali, ni matunda ya ziara ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoifanya katika nchi za Ubelgiji na nchi za Kiarabu hivi karibuni.
Dkt. Nchemba aliwahakikishia wawekezaji hao tarajiwa, kwamba Serikali itaendelea kuboresha sera za uwekezaji na kuwatoa hofu kwamba Serikali ina sera za uwekezaji za uhakika, za kuvutia na zinazotabirika ili iweze kushiriki kikamilifu katika biashara za kimataifa, kikanda na kukidhi soko la ndani.
Alisema kuwa amani na usalama vilivyopo nchini, upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kuwekeza, uwepo wa idadi kubwa ya walaji likiwemo soko la ndani na soko la ukanda, ni fursa nyingine itakayowawezesha wawekezaji hao kupata faida katika uwekezaji wao.
Wakizungumza katika kikao hicho, wawekezaji hao walipongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuhamasisha uwekezaji pamoja na kuweka mazingira mazuri na rafiki ya uwekezaji na ufanyaji biashara.
Walisema kuwa wamekuja nchini kukutana na wadau zikiwemo Wizara na Taasisi mbalimbali ili kujifunza zaidi namna watakavyowekeza mitaji na teknolojia kwenye sekta za kilimo, uzalishaji wa umeme, uchakataji madini, mafuta na gesi.
Mwenyekiti wa wawekezaji hao Bw. Lanre Akinola, alisema kuwa katika miaka michache ijayo, Tanzania inatabiriwa kuwa itakuwa na uchumi imara na wenye nguvu zaidi kutokana na kutarajia kupata wawekezaji wengi kutoka Uingereza na Norway, hatua itakayo kuza uchumi pamoja na kuzalisha ajira kwa wananchi.