Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutatua changamoto mbalimbali za wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo ili kuchochea biashara katika soko hilo linalotegemewa na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Dkt. Nchemba ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya ghafla katika Soko hilo akiambatana na Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Mhe. Mussa Azan Zungu, Mkuu wa Wiaya ya Ilala, Bw. Ng’wilabuzu Ludigija na Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA
Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo walieleza changamoto zao mbalimbali zinazowakabili ikiwemo madai ya kushuka kwa biashara ya nje kutokana na ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa wafanyabishara wa kigeni, ukaguzi ambao walidai si rafiki.
Walisema kuwa wafanyabiashara kutoka nje wanasumbuliwa kwa kudaiwa kuwa risiti wanazopewa na wafanyabiashara baada ya kununua bidhaa hazikuwa sahihi na kuzuiwa mizigo yao hali inayosababisha usumbufu kwa wageni na kumwomba Mhe. Waziri Nchemba aingilie kati ili kufufua biashara katika Soko hilo.
Aidha, Wafanyabiashara hao waliiomba Serikali iongeze kiwango cha mfanyabiashara kusajiliwa kuwa mlipakodi wa VAT kutoka Shilingi milioni 100 hadi Shilingi milioni 500 ili kusisimua biashara zao na kuongeza mzunguko wa fedha utakaowasaidia kukua na kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Ili kupunguza changamoto za kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali, wafanyabishara hao walipendekeza kodi zote ziwe zinatozwa bandarini wakati mizigo inapoingia nchini na kuacha biashara katika Soko la Kariakoo iendelee bila bughudha za masuala ya kodi.
Aidha, Wafanyabiashara hao waliwalalamikia baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wasio waaminifu wanaotumia mwanya wa makosa yanayofanywa na baadhi ya wafanybiashara kudai rushwa na kuikosesha Serikali mapato.
Naibu Spika na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mhe. Mussa Azan Zungu alimwomba Mhe. Waziri Nchemba, kuwachukulia hatua kali watumishi hao wasio waaminifu wanaotumia nafasi zao kujinufaisha kwa kudai na kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara.
Aidha, Mhe. Zungu aliishauri Serikali ipunguze kiwango cha kodi ya mapato (VAT) ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi husika kwa urahisi na hiari zaidi hatua ambayo itakuza biashara na faida kwa wafanyabiashara nchini.
Akijibu hoja za wafanyabiashara hao waliokuwa wakimshangilia mara kwa mara, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, aliiagiza TRA kukutana na wafanyabiashara hao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Alisema kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameelekeza mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara nchini yaboreshwe ili kundi hilo liweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kukuza ajira.
Aliahidi kuwa katika mwaka wa fedha ujao wa 2023/2024 kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kikodi ikiwemo kupunguza VAT na kuja na utaraibu mzuri utakaohamasisha na kukuza biashara nchini.
Aidha, aliahidi kuwa Serikali itaongeza kiwango cha masharti ya wafanyabiashara wanaostahili kusajiliwa kwenye VAT kutoka kiwango cha sasa cha VAT cha Shilingi milioni 100 na kuwekwa kiwango kipya mwaka mpya wa bajeti utakapofika kwa sababu kiwango hicho cha sasa ni cha chini ikilinganishwa na ukubwa wa biashara zinazofanyika.
Dkt. Nchemba aliiagiza pia TRA kutozuia mizigo ya wafanyabiashara wa kigeni wanaonunua bidhaa zao katika Soko la Kariakoo na kuwataka washughulike na wafanyabiashara wasiowaaminifu waliotenda makosa husika kwa kuwa mifumo ya ndani ya nchi haiwahusu wafanyabiashara hao.
Katika hatua nyingine, aliwataka wafanyabiashara hao kuwa waaminifu na kufanyabiashara kwa kufuata misingi mizuri iliyowekwa ikiwemo kutoa risiti halalali zinazolingana na bidhaa walizouza ili kuepuka usumbufu.
Aidha, Dkt. Nchemba aliwaonya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wasiowaaminifu wanaojihusisha na vitendo vya kudai na kupokea rushwa na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao na kuwataka wafanyabiashara hao kutoa taarifa ya watumishi wa namna hiyo wanaoikosesha Serikali mapato.
Kwa upande wake Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, aliyemwakilisha Kamishna Mkuu katika ziara hiyo ya kushtukiza, Bw. Herbert Kabyemela, aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na wafanyabiashara hao na kubainisha kuwa tatizo kubwa linaloikabili Mamlaka hiyo ni suala la ukosefu wa uaminifu wa wafanyabiashara hususan katika kutoa risiti zinazolingana na bidhaa wanazouza.
Dkt. Nchemba aliwaahidi wafanyabiashara hao kwamba atarejea tena sokoni hapo hivi karibuni kusikiliza kero na changamoto zao na kwamba mkutano huo alioufanya utaleta mabadiliko ili Soko hilo la Kariakoo liendelee kuchangia mapato ya Serikali na uchumi wa wafanyabiashara kwa ujumla