Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusaidia kukuza Sekta Binafsi nchini ambayo itasaidia kuongeza kipato, kukuza uchumi wa nchi na itatoa fursa kwa vijana wengi kujiajiri.
Mhe. Dkt. Nchemba alitoa maagizo hayo leo Oktoba 03, 2023 wakati akiongea na wananchi wa Kilambo, Kata ya Njisi, wilayani Kyela, Mkoani Mbeya, mara baada ya kufanya ziara yake ya kukagua shughuli za kiuchumi na maendeleo katika Kituo cha Forodha cha Pamoja-Kasumulu kilichopo mpakani mwa Tanzania na Malawi.
"Ni lazima tuwe na nidhamu katika kuisaidia sekta binafsi na tuache ubosi katika mitaji ya watu na kama kijana ameamua kuanzisha shughuli yake na hajaisajili msimfungie biashara badala yake mleteeni hiyo leseni ambayo hana, msiharibu mtaji wake ili vijana wengi wajiajiri," alisema Mhe. Dkt. Nchemba
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba aliwataka wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi na kuheshimu sheria za nchi ili kuongeza idadi ya walipa kodi, jambo ambalo litasaidia kushusha viwango vya ulipaji kodi na kuwapunguzia mzigo mkubwa wale wanaolipa kodi na kwamba matamanio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuona viwango vya kodi vinashuka ili kuchochea maendeleo ya kila Mtanzania.
"Natoa rai hapa wakati tunawasisitizia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutekeleza maelekezo ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukusanya mapato kwa weledi na kufuata kanuni, tunawasisitiza pia wananchi mjenge utaratibu wa kulipa kodi, kuheshimu sheria ili tunapokwenda tukilipa wengi, tuweze kushusha viwango vya kodi’’ Aliongeza Mhe. Dkt. Nchemba.
Awali akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya, Mhe. Dkt. Nchemba aliwataka kuhakikisha wanadhibiti na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaofanya biashara za magendo katika mpaka wa Kasumulu, vitendo vinavyoikosesha Serikali mapato.