Na Munir Shemweta WANMM KIBITI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Phillip Mpango amewataka viongozi wa dini nchini kuwafundisha na kulea vijana katika maadili mema pamoja na kuthamini kufanya kazi kihalali.
Dkt. Mpango alisema hayo tarehe 25 Septemba, 2022 katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula katika Jubilee ya miaka 25 ya Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Kibiti na sherehe za kutaburuku kanisa na Altare iliyofanyika Kibiti mkoani Pwani.
Alisema, katika nyakati hizi ni ukweli ulio wazi kuwa kuna mmomonyoko wa maadili katoka jamii, vitendo viovu na mambo yasiyompendeza Mungu kuzidi kuongezeka mambo aliyoyaeleza kuwa siku za nyuma yalikuwa nadra kutokea au kusikika na hivi sasa yanakuwa habari za kila siku na wakati mwingine huonekana ni kawaida.
Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, kushuka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na taifa kwa ujumla, hivyo kunachangia kurudisha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo nchini na kufanya kazi ya kuondoa umasikini kuwa ngumu.
Kupitia hotuba ya Makamu wa Rais, Dkt Mabula alisema, anaamini watu pamoja na viongozi wa serikali na wa vyama vya siasa wakishika mafundisho ya dini pamoja na kuwa na hofu ya mungu maovu mengi yatapungua na nchi kuongozwa vizuri.
Kufuatia hali hiyo, aliomba kwa niaba ya serikali viongozi wa dini wasaidie kulea taifa kimaadili na kuweka mkazo zaidi kwa vijana kwa kuwa wao ni wahanga wakuu wa maovu yanayotendeka na pia ni viongozi wa kesho.
"Tukiwaandaa vyema vijana wetu mustakabali wa taifa letu na watu wake utakuwa kwenye mikono salama na tukishindwa leo tutalia na kusaga meno kesho, uhai wa taifa letu utakuwa mashakani " alisema Dkt Mpango.
Kupitia hotuba hiyo, Dkt. Mpango pia alisisitiza suala la usafi na utunzaji mazingira ambapo aliwaomba viongozi wa kanisa katoliki na madhehebu mengine ya dini kupaza sauti kuhamasisha, ulinzi na uhifadhi wa mazingira katika nchi.
"Katika dini zetu Mwenyezi Mungu alitupatia Dunia nzuri na akatuamuru tuitunze, niwaombe ninyi mlio mawakala wa Mwenyezi Mungu hapa duniani muwaongoze waumini na kuwahimiza kuitunza ekolojia ya nchi yetu nzuri kwa kutunza misitu na vyanzo vya maji, kupanda miti na kufanya usafi wa mazingira wakati wote", alisema Dkt. Mpamgo.
Kuhusu mimba na ndoa za utotoni, Dkt. Mpango aliwaomba viongozi wa dini kukemea mimba na ndoa za utotoni kwa kuwa ni kinyume cha sheria na maadili ambapo alieleza kuwa suala hilo linawanyima fursa watoto wa kike kusoma na kufikia malengo sambamba na kusababisha matatizo ya fistula kwa watoto wa kike na kusisitiza watoto wa kike waachwe wasome ili waweze kufikisha malengo yao.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi aliwapongeza wana Kibiti kwa kuwa na kanisa lililokamilika na kuwashukuru wote walioshirikiana katika ujenzi wa kanisa hilo.
Alisema, ujenzi wa kanisa hilo umechukua muda wa miaka 11 na kueleza kuwa, muda huo umekuwa muda wa kukomaa na kuwataka wana kibiti kuonesha ukakamavu na kumpongeza Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Kibiti Christian Goya Lupindu kwa kujituma.