Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Asisitiza Kujenga Uchumi Shindani wa Viwanda
Oct 29, 2023
Dkt. Mpango Asisitiza Kujenga Uchumi Shindani wa Viwanda
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akizungumza leo tarehe 28 Oktoba, 2023 akihitimisha rasmi Maonesho ya Nne ya Wajasiriamali ya Shirika la Viwanda vidogo vidogo (SIDO) yaliyofanyika katika Viwanja vya Sabasaba katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, mkoani Njombe.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango amesema Mpango wa Taifa wa Maendeleo tunaoutekeleza hivi sasa unatutaka tukuze uchumi pamoja na Ajira zinazotokana na viwanda katika Pato la Taifa.

Amesema hayo tarehe 28 Oktoba, 2023 akihitimisha rasmi Maonesho ya Nne ya Wajasiliamali ya Shirika la Viwanda vidogo vidogo (SIDO) yaliyofanyika katika Viwanja vya Sabasaba  katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, mkoani Njombe.

" Hivi sasa mchango wa Sekta ya Viwanda ni asilimia 7.1 tunatamani tufikie asilimia 9 ifikapo mwaka 2025 hadi 2026", amesema Mhe. Dkt. Mpango.

Mhe. Dkt. Mpango amesisitiza kuwa, tafiti zina umuhimu mkubwa sana katika kukuza matumizi ya teknolojia mbali mbali kwenye uzalishaji na uongezaji thamani wa  bidhaa na mazao.

Aidha, Tume ya Madini ambayo pia ilishiriki maonesho hayo imeelekezwa kufanya utafiti ili kujua madini yapi yanapatikana eneo gani? na kuhakikisha takwimu mbali mbali zinapatikana hapa nchini ili kuongeza Pato la Taifa.


Katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Mpango ameeleza kufurahishwa kwake na kauli mbiu ya maonesho hayo inayosema "Kwa Pamoja tujenge Viwanda kwa Uchumi na Ajira  endelevu" na kusema, Kauli mbiu hii iwahamasishe watu wote hasa vijana kuingia kwenye Sekta ya Kilimo, Viwanda na Biashara.

Akizungumza katika maonesho hayo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe amesema Maonesho ya Nne ya Wajasiliamali yamekuwa na ongezeko  kubwa la washiriki ambapo mwaka 2018 walihudhuria Wajasiliamali 582 yalipofanyika  kwa mara ya kwanza Mkoani Simiyu na mwaka 2023 idadi ya  washiriki imeongezeka kufikia Washiriki 628.

Hafla ya kilele cha maonesho hayo ambayo yamefikia tamati tarehe 28 Oktoba, 2023, yamehudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Sekta Binafsi, Viongozi wa dini, Wajasiliamali pamoja na Wananchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi