Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameongoza majadiliano ya Tanzania na Wawekezaji mbalimbali wenye nia ya kuwekeza katika Mradi wa Umwagiliaji wa Bonde la Mara, majadiliano yaliyofanyika katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika mwaka 2022 linalofanyika Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.
Akizungumza katika majadiliano hayo, Makamu wa Rais amesema Tanzania ni sehemu sahihi zaidi ya uwekezaji kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa ni lango muhimu zaidi kibiashara kwa nchi za Afrika Mashariki zenye watu zaidi ya milioni 300 pamoja nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) zenye watu zaidi ya milioni 450.
Amesema uwepo wa ardhi ya kutosha na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo kikubwa pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo inatoa ishara ya mazingira rafiki ya uwekezaji. Amesema Tanzania ina hekta milioni 44 zilizoainishwa kwa ajili ya kilimo, na takriban hekta milioni 10.8 pekee zinazolimwa.
Ameongeza kwamba eneo linalofaa kwa umwagiliaji linakadiriwa kuwa hekta milioni 29.4 na takriban asilimia 2.4 pekee zimetumika.
Pamoja na hayo, Makamu wa Rais ametaja juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan zenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji kama vile uboreshaji wa miundombinu ikiwemo reli na barabara, bandari, usafiri wa anga pamoja na maboresho katika upatikanaji wa nishati ya uhakika.
Makamu wa Rais amesema licha ya janga la Uviko-19, miradi ya uwekezaji kutoka mataifa ya nje iliosajiliwa nchini Tanzania imeongezeka mara tano zaidi hadi kufikia Dola za Marekanj bilioni 2.2 mwaka 2021 kutoka Dola za Marekani milioni 454 mwaka 2020.
Awali akiwasilisha mradi huo kwa wawekezaji, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa amesema mradi huo unatarajia kuimarisha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, ufugaji na uvuvi pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo katika eneo hilo.
Aidha, Mndolwa amesema mradi utaongeza kipato kwa wakulima wadogo wanaoishi maeneo hayo pamoja na kuongeza ajira na uzalishaji wenye tija.
Mradi wa Umwagiliaji wa Bonde la Mara unatarajiwa kutekelezwa katika wilaya ya Serengeti, Tarime na Butiama mkoani Mara.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameongoza majadiliano na wawekezaji juu ya mradi wa ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Mangapwani unaotarajiwa kutekelezwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema mradi huo unaungwa mkono na dhamira kubwa ya kisiasa na miongoni mwa miradi inayopewa kipaumbele na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa lengo la kujenga Uchumi wa Bluu pamoja na kubadilisha Zanzibar kuwa kitovu cha usafirishaji kati ya Kaskazini na Kusini mwa Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nahaat Mohammed Mahfoudh amesema lengo la mradi huo ni kuifungua zaidi Zanzibar kiuchumi na kuwa kiungo muhimu cha biashara ya usafirishaji wa bahari kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Ameongeza kwamba Bandari hiyo inalenga kuhudumia mizigo mbalimbali ya ndani, kikanda na kimataifa na kuwa kichocheo cha kujenga uchumi wa viwanda utakaopelekea kuongezeka kwa ajira na mapato nchini.
Mradi wa Bandari wa Mangapwani ni mradi jumuishi ambao unataorajiwa kuwa na gati ya makontena, mafuta na gesi, chelezo na maeneo huru.
Makamu wa Rais anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika kwa mwaka 2022 linalofanyika Jijini Abidjan Nchini Ivory Coast.