Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Mpango Akutana na Kuzungumza na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo
Sep 06, 2023
Dkt. Mpango Akutana na Kuzungumza na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Geraldine Mukeshimana, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 06 Septemba, 2023.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 06 Septemba, 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Geraldine Mukeshimana. Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es salaam.

 

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango amesema Tanzania itaendelea kutoa mchango wake katika Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ili kuwezesha utekelezaji mbalimbali wa miradi unaofanywa na mfuko huo. Amesema mageuzi katika sekta ya kilimo ni kipaumbele cha Serikali ya Tanzania kwa kuwa inatambua umuhimu wake katika uchumi wa nchi. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Geraldine Mukeshimana pamoja na ujumbe aliofuatana nao mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam. 

Makamu wa Rais ametoa wito kwa IFAD kuona umuhimu wa kuongeza eneo la mradi wa urejelezaji ardhi katika maeneo yanayokabiliwa na ukame Tanzania bara na Zanzibar. Pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji kulingana na uwekezaji halisi wa miradi ili iweze kutekelezwa kwa wakati.

 

Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa IFAD kushirikiana na Tanzania katika tafiti za kina zitakazowezesha matumizi ya ardhi katika maeneo yenye ukame husasani maeneo ya kanda ya kati ya nchi ili iweze kutumika katika kilimo.  Pia amesema ni muhimu kuweka mkazo katika miradi itakayowezesha matumizi sahihi ya rasilimali za majini kama vile baharini na katika maziwa ili kwenda sambamba na vipaumbele vya nchi katika sekta ya uchumi wa buluu.

 

Kwa Upande wake Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Geraldine Mukeshimana amesema Tanzania imekuwa ni mdau muhimu katika mfuko huo kwa kuwa mchangiaji mzuri na hivyo kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali. 

 

Amesema kutokana na athari za migogoro ya kimataifa na UVIKO-19 iliyosababisha ukosefu wa chakula katika maeneo mengi, IFAD inalenga kuhamasisha uchangiaji wa rasilimali fedha kutoka kwa nchi washirika ili iweze kutoa mchango wake katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi